Dar es Salaam. Nia njema ya kuokoa uhai wa mdogo wake aliyekuwa karibu kuchomwa kisu, ndiyo iliyogeuka kuwa mwisho wa maisha ya Lina Kabamba, anayedaiwa kuuawa kwa kisu ambacho awali hakikukusudiwa kwake.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo lililoibua simanzi kupitia mitandao ya kijamii, kilichomponza Lina ni uamuzi wake wa kusuluhisha mzozo wa wadogo zake wawili, hasa pale mmoja alipoonekana kutaka kumchoma kisu mwenzake.
Lina ambaye ni mama wa watoto wanne na mke wa Chriss Kabamba, aliyefunga naye ndoa mwezi mmoja uliopita, alipoteza maisha kwa kuchomwa kisu, saa 7 mchana wa Machi 20, 2026 nyumbani kwao, Rynes, Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Akisimulia tukio hilo, mume wa Lina, Kabamba, anasema shemeji zake hao, walikuwa katikati ya mzozo, uliosababisha mkewe akaingilie kati kuamulia, aliishia kuchomwa visu na kupoteza maisha.
“Siku hiyo nyumbani alikuwepo mama yangu (mkwewe Lina) na mdogo wake na Lina wa kike ambaye ndiye alipiga kelele kuomba msaada kwa majirani baada ya mdogo wao mwingine kufanya mauaji hayo,” anasema.
Katika mitandao ya kijamii, anasema inapotoshwa kuwa aliyemchoma kisu Lina ana matatizo ya akili, lakini uhalisia ni kijana mwenye umri wa miaka 19 na ni shemeji yake na hana tatizo la afya ya akili kama inavyodaiwa.
“Ana akili timamu, ulitokea mzozo hapa nyumbani, yeye na ndugu yake mwingine, mke wangu akaingia kuamulia, ndipo likatokea hilo lililotokea. Taarifa zaidi mkitaka mtapewa na OCD wa Kigamboni ndiye anafuatilia suala hili,” anasema Kabamba.
Hata hivyo, shuhuda mwingine ambaye ni mdogo wa Lina, akiwa nyumbani kwa marehemu Kigamboni, alikataa kuzungumza kwa kina kuhusu tukio hilo, kwa kile alichofafanua, yote yako polisi kwa uchunguzi.
Machache aliyoeleza ni kuhusu dada yake kuacha watoto wanne na mume, aliyefunga naye ndoa mwezi mmoja uliopita na sherehe yao ya harusi ilifanyika katika moja ya kumbi za harusi zilizopo Sinza, Dar es Salaam.
“Kama familia hatujaamua kulizungumzia hili suala, kuna vitu vingi vinazungumzwa mitandaoni ambavyo si vya kweli, hata hivyo OCD wa Kigamboni ndiye anayeweza kulizungumzia,” anasema shuhuda huyo.
Alipotafutwa OCD wa Kigamboni, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yeye si msemaji wa Polisi, akielekeza atafutwe Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.
Muliro alipoulizwa, alikiri kutokea kwa tukio hilo ambalo alisema tayari mtuhumiwa amekamatwa na upelelezi unaendelea kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
“Ni kweli tukio hilo limetokea Kigamboni, ni la Domestic Violence (ukatili wa majumbani) na mtuhumiwa amekamatwa,” alisema Muliro.
Baadhi ya majirani wa marehemu, wamesimulia walivyoanza kusikia kelele za mdogo wa marehemu na mkwewe waliokuwa wanaomba msaada baada ya tukio.
“Kulitokea kelele za kuomba msaada, tulipofika eneo la tukio tukamkuta, mtuhumiwa anasafisha damu mwenyewe,” anasema jirani mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Jirani mwingine, anasema alikuwa akimuona kijana huyo mdogo wake Lina aliyetenda tukio kwa takriban mwezi mmoja, aliishi nyumbani na familia hiyo.
“Hakuwa na tatizo la akili, ila kuna tetesi kwamba kulikuwa na mgogoro, yule kijana ambaye naye anafanya kazi za biashara mtandaoni kama alivyokuwa dada yake Lina, kuna hela alichukua ya mteja hakumpelekea bidhaa,” anasema jirani huyo.
Kwa sababu hiyo, anadai Kabamba na Lina walimtaka arudishe fedha kwa mwenyewe, ambayo inadaiwa kuwa ni Sh1.5 milioni. Hata hivyo, Kabamba amekataa taarifa hizo, akisema si za kweli.
Jirani huyo, anafafanua kuwa siku ya tukio, mdogo wa Lina wa kike alikuwa akimueleza kaka yao arudishe pesa ya mteja aliyochukua.
“Alimueleza kwa nia njema, ndipo mtuhumiwa akapaniki na kuchukua kisu kwa lengo la kumchoma. Lina alivyoona akaingilia kati na akachomwa yeye,” anasema.
Anasema majirani walipokwenda kutoa msaada walimkuta mtuhumiwa akisafisha damu mwenyewe, ndipo wakatoa msaada na kufanikisha mtuhumiwa kukamatwa.
Kwa mujibu wa mume wa marehemu, mwili wa Lina kesho Jumanne Machi 24, 2026 saa nane mchana utatolewa mochwari na kupelekwa nyumbani kwake na usiku wa siku hiyo kutakuwa na mkesha wa maombolezo.
Jumatano saa 5 asubuhi mwili utatolewa nyumbani kwenda kanisa la KKKT Kisiwani ambako itafanyika ibada ya misa ya kuaga kabla ya maziko yatakayofanyika kwenye makaburi ya Kisota, Kigamboni.
