Muya ataka mechi za kirafiki Coastal

KOCHA wa Coastal Union Mohamed Muya ameweka wazi mkakati wake kuelekea kipindi hiki cha mapumziko, huku akisisitiza umuhimu wa kucheza mechi za kirafiki ili kujiweka sawa kabla ya kurejea kwenye ushindani.

Akizungumza na Mwanaspoti alisema kuwa, mapumziko haya hayapaswi kuwa ya kupoteza muda, bali ni fursa ya kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika michezo iliyopita na kuimarisha kikosi kwa ujumla.

Muya alisema, mechi za kirafiki zitawasaidia wachezaji wake kubaki katika kiwango kizuri cha ushindani pamoja na kuongeza muunganiko ndani ya timu.

Aliongeza kuwa, kupitia michezo hiyo, atapata nafasi ya kuwapa dakika zaidi baadhi ya wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kutosha kwenye mechi za ligi.

“Eneo ambalo nitakwenda kulifanyia kazi ni mbele hasa kwa washambuliaji kumekuwa na changamoto kidogo ya kutumia nafasi zinazopatikana.

“Timu imekuwa ikitengeneza nafasi nyingi kweli,lakini tatizo limekuwa kwenye umaliziaji, jambo ambalo nataka kulifanyia kazi kwa kina katika kipindi hiki ili tunaporudi timu iweze kupata matokeo mazuri.

“Kuhusu swala la mechi nataka kuangalia kama tutapata mbili au tatu za kirafiki na timu yoyote iwe ya Ligi Kuu au Championship lengo ni kujiweka sawa.”

Mara ya mwisho Coastal kubeba pointi tatu ilikuwa ni mechi dhidi ya Tanzania Prisons ambapo iliwatandika mabao 1-4 ugenini.

Kikosi hicho ni wazi kwamba hakijaanza vyema msimu ukilinganisha na rekodi ilizonazo kwani imecheza mechi 16 inashika 13, imeshinda tatu,sare sita na kupoteza saba.