KOCHA wa Prisons, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, amesema kuwa kikosi hicho hakitakuwa na muda wa mapumziko kwani anahitaji kufanyia kazi eneo la utulivu kwa wachezaji wake.
Nsajigwa alichukua nafasi hiyo baada ya klabu hiyo kuachana na Zedekiah Otieno kufuatia mfululizo wa matokeo mabaya, kwa sasa ameiongoza timu hiyo katika mechi tatu za Ligi Kuu.
Tangu akabidhiwe kikosi hicho, bado hajapata nafuu ya matokeo huku akipata suluhu dhidi ya Azam na kupoteza mbele ya Yanga 0-1 na Singida Black Stars 1-2.
Matokeo yaliyozidi kuiweka kikosi hicho kwenye hali mbaya, kikishika nafasi ya 15, ikiwa imecheza mechi 17, ikishinda mitatu, sare nne na kupoteza 10, ikivuna jumla ya pointi 13.
Akizungumza na Mwanaspoti, alisema kuwa katika michezo iliyopita kumekuwa na changamoto ya wachezaji kukosa utulivu wanapokuwa uwanjani, jambo ambalo limekuwa likiathiri matokeo ya timu.
Alieleza kuwa utulivu ni sehemu muhimu ya mafanikio kwani unasaidia wachezaji kufanya maamuzi sahihi katika nyakati muhimu za mchezo.
“Natarajia kutumia muda huu kuhakikisha wachezaji wanajengewa uwezo wa kuwa watulivu hata wanapokuwa chini ya presha.
“Baada ya sikukuu, timu itarejea rasmi mazoezini kwa lengo la kujiandaa vyema kwa michezo inayofuata na mazoezi hayo yatakuwa na malengo maalum ya kuboresha nidhamu ya mchezo pamoja na kuimarisha uwezo wa kiakili kwa wachezaji.
Kocha huyo amebainisha kuwa anahitaji kuona mabadiliko chanya kutoka kwa wachezaji wake ili waweze kushindana kwa kiwango cha juu zaidi.
Baada ya mapumziko ya FIFA, Prisons itaanza na mechi ngumu ugenini dhidi ya Yanga, Jumamosi Aprili 4, saa 12:30 jioni.