Sand Heroes wasitisha mazoezi kufuatia CECAFA kuahirisha mashindano

BAADA ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na kati (CECAFA) kuahirisha mashindano ya soka la ufukweni, timu ya Taifa ya Ufukweni Zanzibar maarufu Zanzibar Sand Heroes imesema bado inasubiria kamati itoe maelekezo ili waanze mazoezi.

Kauli hiyo imetolewa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kijo Nadir Nyoni wakati akizungumza na Mwanaspoti ambapo alisema wamecha kufanya mazoezi baada ya CECAFA kutoa taarifa ya kuahirishwa kwa mashindano hayo yaliyopangwa kufanyika Mombasa nchini Kenya kuanzia Julai 16 hadi 20 mwaka huu.

Nchi saba zimefuzu kushiriki mashindano hayo ambazo ni wenyeji Kenya, Burundi, Malawi, Seychelles, Tanzania, Uganda na Zanzibar.

“Kipindi hiki hakuna mashindano, hivyo hakuna programu yoyote ya mazoezi inayoendelea, tunasubiri kamati ituelekeze cha kufanya baada ya mashindano kuahirishwa.

“Hatuwezi kuendelea na mazoezi wakati hatufahamu mashindano yatafanyika lini na wala sisi hatuna mashindano mengine, hivyo inatuwia vigumu,” alisema Kijo. Kijo alisema kuacha kufanya mazoezi kutaathiri kikosi kwani kukaa muda mrefu bila ya wachezaji kujishughulisha si vizuri.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Julai  13, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA, Auka Gecheo, ilieleza mashindano hayo yameahirishwa kufuatia ombi kutoka kwa Serikali ya kaunti ya Mombasa na mamlaka husika za serikali ya kitaifa.

Hivyo, CECAFA ilisema itatangaza tarehe mpya kuambatana na ratiba za kimkakati za Serikali ya kaunti ya Mombasa na kufanya kazi kwa karibu na washirika wa ndani.