Serikali yaonya watakaoficha mafuta kusubiri yapande bei

Dodoma. Serikali imesema haitawavumilia wafanyabiashara wa mafuta ya vyombo vya moto ikiwamo petroli, watakaotumia mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati, kuficha bidhaa hiyo wakisubiri ipande bei, ikisisitiza vitendo hivyo vinahatarisha upatikanaji wa nishati kwa wananchi.

Sambamba na hilo, imeagiza kuundwa kwa kamati maalumu ya kufuatilia mwenendo wa uingizaji wa mafuta nchini, kuhakikisha yanafika kwa wakati kwa mujibu wa mikataba iliyopo.

Serikali inatoa onyo hilo ikiwa ni mwezi mmoja tangu kuanza kwa vita katika ukanda wa Mashariki ya Kati, vinavyohusisha mataifa ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ambavyo vinatishia hatari ya kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

Uwezekano wa kupanda kwa bei hiyo, unatokana na eneo la Mashariki ya Kati kuwa kitovu cha uzalishaji na usafirishaji wa mafuta duniani, hivyo vita huenda ikaathiri hilo.

Tayari vita hiyo imeshazalisha hatari kwa njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta ya Strait of Hormuz, inayounganisha Ghuba ya Uajemi na masoko ya dunia. Takribani asilimia 20 ya mafuta yote duniani hupita hapo kila siku.

Machi 21, mwaka huu, Rais wa Marekani, Donald Trump alitoa saa 48 kwa Iran, kuufungua mlango wa bahari wa Hormuz, akitishia kuangamiza miundombinu ya umeme ya Iran iwapo haitaruhusu meli kupita bila masharti.

Trump alisema Iran ina hadi saa 23:44 GMT Machi 21, (8:44 usiku kwa saa za Afrika Mashariki) hadi leo Machi 24, kutekeleza agizo hilo.

Hata hivyo, Serikali ya Iran imejibu agizo hilo ikionya itashambulia miundombinu ya mafuta inayohusishwa na Marekani katika eneo la Ghuba iwapo itashambuliwa.

Mvutano huo, umeongeza hofu ya usalama wa nishati duniani, hasa kutokana na umuhimu wa Strait of Hormuz, ambayo hupitisha sehemu kubwa ya mafuta yanayosafirishwa kimataifa.

Machi 4, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema siku chache tangu kuanza kwa vita hiyo, bei ya mafuta imepanda kwa takriban asilimia 13, huku akitoa tahadhari ya hatari za uchumi wa dunia.

Onyo hilo la kuficha mafuta, limetolewa leo, Jumatatu Machi 23, 2026 na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, wakati wa kikao na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo zinazohusika na sekta ya mafuta, uliofanyika jijini Dodoma.

Ametaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kufanya ukaguzi wa kina katika maghala ya kuhifadhi nishati hiyo, ili kuhakikisha hakuna mfanyabiashara anayeficha mafuta kwa lengo la kusubiri bei kupanda.

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa uhakika katika maeneo yote ya nchi, licha ya changamoto zinazotokea katika soko la dunia.

“Hatutarajii kuona mfanyabiashara yeyote akificha mafuta kwa kisingizio cha kusubiri bei kupanda. Nchi ina akiba ya kutosha na Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bila vikwazo,” amesema.

Ameisisitiza Ewura kuongeza ufuatiliaji katika maghala na vituo vya mafuta ili kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyoweza kusababisha upungufu wa nishati hiyo sokoni.

Hatua nyingine ya kuimarisha usalama wa upatikanaji wa mafuta, Ndejembi ameagiza kuundwa kwa timu maalumu ya kufuatilia mwenendo wa uingizaji wa mafuta nchini.

Timu hiyo, ametaka ihusishe wataalamu kutoka Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Ewura, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na vyombo vya ulinzi na usalama.

Amesema jukumu la timu hiyo ni kufuatilia hatua kwa hatua mafuta yote yaliyoagizwa nje ya nchi ili kuhakikisha yanafika nchini kwa wakati kulingana na mikataba iliyopo.

“Hali ya biashara ya mafuta duniani si ya kuridhisha kwa sasa. Baadhi ya nchi zimeanza kuona bei za mafuta zikiongezeka maradufu na wafanyabiashara wengine wanaweza kushawishika kupeleka mafuta kwenye masoko yenye bei kubwa zaidi. Hatutaruhusu mikataba tuliyoingia ikikiukwa,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, James Mataragio amesema Tanzania ina akiba ya kutosha ya mafuta itakayotosheleza mahitaji ya nchi hadi Julai 2026.

Ameeleza Serikali ilichukua hatua mapema kwa kushirikiana na taasisi zake ili kuhakikisha mafuta yanaagizwa kwa wakati na kwa gharama himilivu kwa wananchi.

“Tunafuatilia kwa karibu mafuta yote yaliyopo njiani kuja nchini na kuyasimamia masoko ya ndani ili kuhakikisha, hakuna mfanyabiashara anayechukua fursa ya changamoto za kimataifa kupandisha bei kiholela,” amesema.

Awali, Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Simon ameeleza hali ya upatikanaji wa mafuta nchini kwa sasa ni salama, akieleza kuwa, kiasi cha mafuta kilichopo ndani ya nchi na kilichopo njiani kinatosheleza mahitaji kwa muda mrefu.

Amesema kuna petroli lita milioni 474 zinazoweza kukidhi mahitaji ya siku 78, dizeli lita milioni 392 zinazotosheleza siku 50, na lita milioni 55 za mafuta ya ndege zinazotosheleza siku 91.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, amesema Serikali ilishasaini mikataba mapema na wazabuni wa mafuta ili kuhakikisha uingizaji wake unafanyika bila usumbufu.

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Andilile amesema kwa sasa soko la mafuta nchini linaendelea kuwa tulivu bila mfumuko wa bei.

Amesema mamlaka hiyo, itaendelea kushirikiana na waagizaji na wauzaji wa mafuta ili kuhakikisha changamoto zozote zinatatuliwa kwa haraka na kuzuia vitendo vya kuficha mafuta vinavyoweza kuathiri upatikanaji wake kwa wananchi.