Serikali Yatangaza Nafasi za Kazi 630, Mwisho wa maombi Aprili 4, 2026

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza jumla ya nafasi 630 za kazi kwa Watanzania wenye sifa na uwezo wa kujaza nafasi mbalimbali katika taasisi za serikali (MDAs & LGAs) pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Fungua link hii kusoma zaidi >>> NAFASI ZA KAZI MDAs NA LGAs 22-03-2026

Kwa mujibu wa tangazo hilo lenye Kumb. Na. JA.9/259/01/C/24 la tarehe 22 Aprili 2026, nafasi hizo zinajumuisha kada tofauti zikiwemo Walimu wa Elimu Maalum (nafasi 7), Mwandishi Mwendesha Ofisi Daraja la II (nafasi 243), Daktari wa Mifugo Daraja la II (nafasi 1), Mkadiriaji Ujenzi Daraja la II (nafasi 55), pamoja na Madereva Daraja la II (nafasi 296).

Aidha, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza nafasi za wakufunzi wasaidizi katika fani mbalimbali zikiwemo Uandaaji wa Chakula (Food Production) (nafasi 5), Ushonaji na Ubunifu wa Mitindo (Tailoring and Fashion Design) (nafasi 10) pamoja na Uchomeleaji na Utengenezaji wa Vyuma (Welding and Metal Fabrication) (nafasi 13).

Waombaji wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania wenye sifa zinazotakiwa kwa kila nafasi, ikiwa ni pamoja na elimu, mafunzo ya kitaaluma na vyeti vinavyotambuliwa na mamlaka husika. Aidha, maombi yote yanapaswa kuwasilishwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa ajira (Recruitment Portal) kupitia anuani ya https://portal.ajira.go.tz/.

Tangazo hilo limesisitiza kuwa waombaji wanapaswa kuambatisha nyaraka muhimu ikiwemo vyeti vya elimu vilivyothibitishwa, cheti cha kuzaliwa na barua ya maombi iliyoandikwa na kusainiwa. Vilevile, hati kama “testimonials”, “provisional results” na matokeo ya mitihani (FORM IV na VI results slips) hazitakubaliwa.

Serikali pia imetoa masharti ya jumla ikiwemo umri wa waombaji kutokuzidi miaka 45, huku ikihimiza watu wenye ulemavu kuomba nafasi hizo na kuainisha hali zao katika mfumo wa maombi. Mwisho wa kutuma maombi umewekwa kuwa tarehe 04 Aprili 2026.

Fungua link hii kusoma zaidi >>> NAFASI ZA KAZI MDAs NA LGAs 22-03-2026