Dar es Salaam. Benki ya Stanbic imeibuka kinara kwa kushinda tuzo tatu za kimataifa za Benki Bora ya Kimataifa kwa Wateja Maalumu, Benki Bora kwa Kizazi Kijacho, na Benki Bora kwa Huduma kwa Wateja.
Ushindi huo unaonesha mchango wake katika kusaidia wateja wa Tanzania kujenga, kukuza na kulinda ukwasi wao kwa mtazamo wa muda mrefu na vizazi vijavyo.
Tuzo hizo zilitolewa na jarida la Euromoney baada ya tathmini ya kina iliyofanywa na jopo huru la wataalamu wa sekta ya kibenki, na zilitangazwa katika hafla ya Euromoney Private Banking Awards 2026 iliyofanyika jijini London, Uingereza, mwishoni mwa wiki.
Utambuzi huu unakuja wakati uchumi wa Tanzania ukiendelea kukua, ukiwa na makadirio ya ukuaji wa kati ya asilimia 5 hadi 6 kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, sambamba na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi na uwekezaji. Hali hii imechochea ukuaji wa ukwasi, hasa kwa wajasiriamali na biashara za kifamilia.
Tuzo ya benki bora ya kimataifa kwa wateja maalumu inaonesha uwezo wa Stanbic kuwaunganisha wateja wake na masoko ya kimataifa pamoja na fursa za uwekezaji, hivyo kuwawezesha kukuza ukwasi wao ndani na nje ya mipaka ya nchi. Hii ni mara ya pili mfululizo kwa benki hiyo kupata utambuzi huu, jambo linaloonesha ushawishi wake katika kutoa suluhisho za kifedha za kimataifa.
Tuzo ya benki bora kwa kizazi kijacho inaangazia mpango wa kuwaandaa warithi na vijana kusimamia mali kwa uwajibikaji, hasa wakati biashara nyingi za kifamilia zinaanza kupokelewa na kizazi kipya.
Tuzo ya benki bora kwa huduma kwa wateja inaonesha umuhimu wa mahusiano ya muda mrefu na ushauri unaolengwa mahususi kwa kila mteja katika kumsaidia kufanya maamuzi ya kifedha yenye uzito kwa kipindi cha muda mrefu.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mtendaji Mkuu wa Benki ya Stanbic Tanzania, Manzi Rwegasira, amesema tuzo hizo zinaonesha mabadiliko mapana katika namna mali zinavyoundwa na kudumishwa nchini.
“Kwa Tanzania, mali mara nyingi hazibaki kwa mtu mmoja pekee. Zinahudumia familia, zinaendeleza biashara na zinachangia jamii. Kadri mali zinavyozidi kuongezeka, ndivyo umuhimu wa kuzipanga, kuzilinda na kuhakikisha zinarithishwa kwa ufanisi kwa vizazi vijavyo unavyoongezeka. Tuzo hizi zinaakisi kazi tunayoifanya kusaidia wateja wetu katika safari hiyo,” amesema.
Licha ya ukuaji mzuri wa uchumi, upatikanaji wa huduma za kifedha nchini bado ni mdogo ukilinganisha na masoko yaliyoendelea, ambapo mikopo kwa sekta binafsi bado inachangia sehemu ndogo ya pato la taifa, kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania.
Hali hii inaonesha fursa kubwa ya kuimarisha suluhisho za kifedha zilizopangiliwa zaidi, zikiwemo ushauri wa uwekezaji, mipango ya mali na usimamizi wa urithi.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Wateja Maalumu wa Benki ya Stanbic, Omari Mtiga, amesema huduma kwa wateja maalum sasa zinaelekezwa zaidi katika kujenga ushirikiano wa muda mrefu na mwendelezo wa kifedha.
“Jukumu letu ni kuelewa safari kamili ya mteja, biashara zake, familia yake na malengo yake ya baadaye. Tunafanya kazi nao kuhakikisha mali zao si tu zinahifadhiwa, bali pia zinarithishwa kwa mpangilio unaoleta uendelevu,” amesema.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja Maalumu Stanbic, Beatrice Kisoka, amesema wateja wengi sasa wanaangalia zaidi ya mafanikio ya sasa.
“Wateja wengi wanazingatia maana halisi ya mali zao kwa familia na vizazi vijavyo. Wanataka kuona mwendelezo, uthabiti na athari ya muda mrefu, na hilo linahitaji mwongozo pamoja na mipango iliyopangiliwa vizuri,” amesema.
Aidha, tuzo hizo zinakuja katika kipindi ambacho Benki ya Stanbic imetajwa kuwa benki bora nchini Tanzania kwa mwaka 2025 na jarida la The Banker, jambo linaloonesha uthabiti wa benki hiyo katika shughuli zake zote.