SAFU ya ushambuliaji ya timu ya JKU inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) imeendelea kujiwekea mikakati kabambe kuhakikisha taji linarudi msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, mshambuliaji wa timu hiyo, Feisal Hilali Nassor amesema JKU ipo Ligi Kuu Zanzibar kwa ajili ya kupambania ubingwa na sio kushiriki.
Alisema ndio maana kila mchezaji wa timu hiyo kipaumbele chake ni kutimiza lengo la timu kwanza, kisha kujipambania mwenyewe.
Feisal alisema, ushindi wa timu ndio taswira nzuri inayompa thamani mchezaji wakati wa utafutaji wake kwa sababu ikifanya vizuri hufanya wachezaji kufuatiliwa.
“Tunacheza ligi kwa kupambania ubingwa na sio kushiriki tu, kwanza malengo ya timu kisha kujipambania mwenyewe ili nizidi kuwa na thamani kwa kila mechi nitakayocheza,” alisema Feisal.
Mshambuliaji huyo msimu huu 2025-2026, amecheza mechi 19 kati ya 20 za Ligi Kuu Zanzibar, huku akifunga mabao manne na asisti nne.
Feisali alisema kati ya mechi 20 ilizocheza JKU, moja alikaa benchi huku akimini mwalimu katumia nafasi hiyo kumpa mapumziko baada ya kufanya kazi kubwa kwenye mechi 19.
Mchezaji huyo alisema, jitahada zake anazofanya anahitaji kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu kwa sababu itamjengea heshima na kuaminika na kila mmoja.
JKU ilichukua ubingwa msimu wa 2023-2024, lakini ikaja kuvuliwa na Mlandege msimu wa 2024-2025. Kwa sasa timu hiyo ipo nafasi ya tano kwenye msimamo wa ZPL ikikusanya pointi 36, tofauti ya pointi mbili ilizonazo kinara wa ligi hiyo Fufuni yenye 38.