Taasisi za fedha zatakiwa kubuni huduma rafiki kwa wanawake

Arusha. Serikali imezitaka taasisi za kifedha nchini kubuni bidhaa na huduma zinazozingatia mahitaji ya wanawake ili kuongeza ushiriki wao katika uchumi rasmi na kuchochea ukuaji wa pato la Taifa.

Wito huo umetolewa leo Machi 23, 2026 jijini Arusha na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Omary, wakati akifungua mkutano wa tatu wa wanawake katika sekta ya fedha ulioandaliwa na Tanzania Women in Finance Association (TAWiFA) chini ya kaulimbiu “Give to Gain: Empowering Tanzanian Women in Finance.”

Balozi Omary amesema taasisi za fedha zinapaswa pia kuimarisha elimu ya kifedha kwa wanawake ili waelewe fursa zilizopo kama bima, soko la mitaji na uwekezaji, hatua itakayowawezesha kupata mitaji, kukuza biashara na kulinda mali zao. Amesema hatua hiyo itachochea ustawi wa familia na kuimarisha uchumi wa taifa.

Amebainisha kuwa wanawake ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini na wanachangia kwa kiasi kikubwa katika biashara na uzalishaji, huku zaidi ya asilimia 50 ya biashara ndogo na za kati (SMEs) wakiziendesha.

Kwa upande wa Serikali, amesema ujumuishaji wa kifedha umeongezeka hadi asilimia 76 kutoka asilimia 65 mwaka uliopita, huku maendeleo ya teknolojia ya fedha yakichangia ongezeko la akaunti zaidi ya milioni 60 kupitia simu za mkononi.

“Wanawake ni zaidi ya asilimia 60 ya watumiaji wa huduma hizi.”

Amesema kati ya mwaka 2022 na 2025, wanawake zaidi ya milioni 1.3 walipata mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh748 bilioni kupitia mifuko ya uwezeshaji. Serikali pia inaendelea kusimamia lengo la angalau asilimia 30 ya wanawake kushika nafasi za juu za uongozi katika taasisi za kifedha.

Awali, Rais wa TAWiFA, Fikky Ntomola amesema mkutano huo unalenga kuwawezesha wanawake na kuwaunganisha ili wachangie kikamilifu katika uchumi. Ameeleza kuwa licha ya wanawake kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania, wanaofikiwa na huduma za kifedha bado ni chini ya asilimia 30.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Saada Mkuya amesema changamoto zilizopo ni pamoja na uwakilishi mdogo wa wanawake katika nafasi za juu na upungufu wa elimu ya kifedha.

Katika hatua nyingine, TAWiFA imeanzisha mfumo wa kidijitali (portal) utakaowawezesha wanawake kuunganishwa, kupata taarifa na kushiriki fursa mbalimbali, ambapo Balozi Omary alizindua rasmi mfumo huo.