Morogoro. Wakati Tanzania ikijivunia kuwa na idadi kubwa ya mifugo, bado inalazimika kutumia zaidi ya Sh23 bilioni kila mwaka kuagiza wastani wa lita milioni 11.6 za maziwa kutoka nje ya nchi.
Hali hiyo inayochangiwa na changamoto za ubora ambapo miundombinu na elimu kwa wadau wa sekta maziwa ni vikwazo vinavyosababisha maziwa kukosa ubora.
Akizungumza katika mafunzo ya wakaguzi wa tasnia ya maziwa mjini Morogoro, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Profesa George Msalya amesema licha ya Tanzania kuzalisha takribani lita bilioni 4.1 za maziwa kwa mwaka, bado kuna pengo la uzalishaji linalosababisha nchi kuendelea kuagiza maziwa kutoka nje ili kukidhi mahitaji ya ndani.
Profesa Msalya amesema changamoto kubwa ni ubora wa maziwa yanayozalishwa na wadau wengi, hasa wa vijijini, hawazingatii viwango vinavyotakiwa, hali inayowafanya walaji wengi kuamini kuwa maziwa ya nje ni bora zaidi kuliko yanayozalishwa nchini.
“Maziwa yetu bado ni bora na hii ya baadhi ya walaji kudhani maziwa yetu sio bora ndio hali inayoathiri moja kwa moja Tanzania kuagiza maziwa nje, lakini viwanda vyetu vya ndani vinasindika maziwa yenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa,” amesema Profesa Msalya.
Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania ina jumla ya viwanda 188 vya kusindika maziwa, vikiwemo vidogo, vya kati na vikubwa, lakini ni vinane pekee vilivyo katika kundi la viwanda vikubwa.
Hata hivyo, viwanda hivyo hupata takribani asilimia 20 tu ya maziwa yanayozalishwa nchini, jambo linalosababisha kushuka kwa uzalishaji wa bidhaa za maziwa kama mtindi, siagi na maziwa yaliyosindikwa.
Akielezea changamoto nyingine, Profesa Msalya amesema miundombinu duni hasa katika maeneo ya vijijini ambako uzalishaji mkubwa wa maziwa unafanyika, imekuwa kikwazo kikubwa cha kufikisha maziwa sokoni na viwandani kwa wakati.
Kwa upande wake, Ofisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Issa Kigonza amesema baada ya mafunzo hayo, wana wajibu wa kuweka mikakati ya kuhakikisha biashara ya maziwa inadhibitiwa na kuondokana na uuzaji holela.
Kigonza amesema bado kuna biashara ya maziwa mitaani isiyofuata utaratibu, hivyo wataendelea kutoa elimu kwa wafugaji na wauzaji ili kuhakikisha maziwa yanaingizwa katika mfumo rasmi na watumiaji wanapata maziwa salama na yenye ubora.
“Tutahakikisha wafugaji wanazingatia usalama wa maziwa kuanzia uzalishaji hadi kwa mlaji, ili kulinda afya za wananchi,” amesema Kigonza.
Kwa mujibu wa wataalamu wa lishe kutoka Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO), mtu mmoja anashauriwa kunywa angalau lita 200 za maziwa kwa mwaka, sawa na mililita 250 kwa siku, kiwango ambacho bado hakijafikiwa na Watanzania wengi.
Kwa upande wake, ofisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mariam Kingu amesema Serikali chini ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya kukuza tasnia hiyo.
Mariam amesema Serikali imeondoa baadhi ya kodi kwenye vifaa muhimu kama matanki ya kuhifadhia maziwa na mitambo ya usafirishaji ili kurahisisha uwekezaji na kuboresha ubora wa maziwa.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa Sh462 bilioni unaolenga kuimarisha tasnia ya maziwa hususan katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoathiri uzalishaji wa mifugo.
Ameongeza kuwa wizara pia imeteua wakaguzi 184 wa tasnia ya maziwa wanaopatiwa mafunzo kwa awamu ili kuhakikisha sheria na sera ya maziwa ya mwaka 2004 inatekelezwa kikamilifu.
Katika jitihada nyingine, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara vijijini ili kurahisisha usafirishaji wa maziwa kutoka mashambani kwenda viwandani na kwa walaji.
