Wanaotumia vibaya vyandarua vya msaada waonywa

Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adamu Malima amekemea tabia ya baadhi ya watu kuchukua vyandarua wanavyogawiwa bure na Bohari ya Dawa (MSD) na kuvigeuza mabanda ya kufugia kuku, ama nyavu za kuvulia samaki.

Kufuatia hilo, Malima amewataka    wakuu wa wilaya zote mkoani humo kufuatilia kwa karibu matumizi sahihi ya vyandarua hivyo.

Malima ameyasema hayo leo Machi 23, 2026 wakati akizindua shughuli ya usambazaji na ugawaji wa vyandarua 1,686,933 linaloendeshwa kwa usimamizi wa MSD,  akisema   kuwa lengo la Serikali ni kutokomeza ugonjwa wa Malaria kufikia asilimia 0 ifikapo 2030.

“Viongozi wenzangu tusione taabu kuhakikisha vyandarua hivi vinatumika kwa usahihi na kwa lengo lililokusudiwa, huenda kuna watu watavichukua na kwenda kufugia kuku ama kuvulia samaki, lazima vyandarua hivi pamoja na afua nyingine vitokomeze Malaria,” amesema Malima.

Amesema ili Malaria itokomezwe ni lazima jamii iuchukie ugonjwa huo, pia, viongozi wa Serikali na wadau wengine washiriki katika kutoa elimu kwa jamii ya namna ya kujikinga kwa kutumia vyandarua kwa usahihi na kufanya usafi wa mazingira yakiwemo mazalia ya mbu.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amewataka wananchi wa Morogoro kujenga tabia ya kufanya vipimo endapo watahisi kuambukizwa ugonjwa wa Malaria na kuacha kunywa dawa za ugonjwa huo bila ya kupima wala kushauriwa na daktari kwani wanaweza kuathiri afya zao.

“Kuna watu wakihisi mabadiliko ya kiafya wanakimbilia kununua dawa za Malaria badala ya kwenda kupima, hiki ni kitu kibaya, kinachosababisha usugu wa vimelea vya ugonjwa huo. Hivyo, pamoja na kugawa vyandarua, MSD mna nafasi ya kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya dawa za Malaria,” amesema Malima.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi ya usambazaji na ugawaji dawa Mkurugenzi wa Logistics kutoka MSD, Hassan Ibrahimu ameahidi kwamba watafanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa kwa kuwa jukumu lao ni kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinafika mahala husika.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adamu Malima akizindua zoezi la usambazaji na ugawaji wa vyandarua mkoa wa Morogoro unaofanywa na bohari ya dawa MSD. Picha Hamida Shariff

“Tumepanga kazi hii ya kusambaza na kugawa vyandarua kwa wananchi tuifanye kwa siku 30 katika halmashauri saba kati ya tisa za Mkoa wa Morogoro na jumla ya kaya 6,908 katika halmashauri hizo wakiwemo wajawazito, wazee na wenye ulemavu, zitapata vyandarua,” amesema Ibrahimu.

Kwa upande wake, mratibu wa Malaria na udhibiti wadudu wadhurifu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Stella Kajange amesema Serikali imeendelea kuweka nguvu katika kupambana na maambukizi ya Malaria ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na 2025/2026 Serikali imetoa Sh19 bilioni kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo, Sh15 bilioni zilisaidia kununua viuatilifu vya kuangamiza mazalia ya mbu na Sh4 bilioni zilitumika kununua pampu za kunyunyuzia vimelea vya wadudu wa Maralia

“Mbali ya kutoa fedha hizo lakini pia Rais Samia Suluhu Hassan ameunda baraza la kutokomeza Maralia pia Wizara ya Afya imeandaa mwongozo wa namna ya kutokomeza Maralia,” amesema Kajange.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya zote za Morogoro, amewahakikishia ushirikiano watendaji wote wa MSD na kuahidi kusimamia kazi hiyo kwa ajili ya kutokomeza Malaria.

Kaulimbiu ya ugawaji vyandarua kwa Morogoro inasema “Ziro Malaria inaanza na wewe, mimi na sisi sote, Tanzania bila Malaria inawezekana”.