Wanne washikwa mkono gofu kimataifa

WAKATI mashindano ya gofu kwa chipukizi Afrika yakianza jana Jumatatu nchini Kenya, Benki ya NCBA imejitolea kuwadhamini watoto wanne watakaoiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo.

Watoto hao wanatarajia kuibeba Tanzania katika mashindano yatakayofanyika kati ya Machi 23 hadi 26 mwaka huu nchini Kenya katika Jiji la Nairobi.

Watoto hao wanaoiwakilisha Tanzania ni Ibrahim Juma, Julius James, Auni Jaffari na Gervas Wilbroda. Hayo yamewekwa bayana na Mkurugenzi Mtendaji wa NCBA Bank Tanzania, Alex Mziray alipozungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza dhamira ya benki hiyo katika kuinua vipaji vya vijana hasa katika gofu.

Alisema wameamua kufanya hivyo kwa sababu wanaamini vijana wakipewa nafasi wanaweza kufika mbali.

“Ni ushahidi kwamba maendeleo ya taifa hayaanzi kwenye takwimu bali yanaanzia kwa watu. Kwa wengine, huu ni mchezo lakini kwao huu ni mwanzo wa safari ya kujenga maisha yao. Kwa wengi wao, hii ni hatua kubwa kutoka kwenye uwanja wa mazoezi hadi jukwaa la kimataifa,” alisema.

Alisema licha ya kuwapo kwa ndoto hizo ili safari ifike mbali ni lazima ipate msukumo, msaada na nafasi ya kukua. “Ndoto bila msaada hubaki kuwa ndoto. Lakini ndoto inapoungwa mkono, hugeuka kuwa mafanikio ndiyo maana sisi tunaingia katika kuhakikisha kila kitu kinafanikiwa,” alisema.

Alisema hili linafanyika kwa sababu wanaamini maendeleo siyo tu ukuaji wa uchumi bali ni uwezo wa mtu mmoja, familia moja au kijana mmoja kubadilisha maisha yake.

“Pale ambapo taasisi zinachagua kuamini katika watu, ndipo hadithi za mafanikio huanza kuandikwa,” alisema.

Mbali na kudhamini watoto hao, pia wamejikita katika kuinua vipaji vingine kwa kutoa udhamini wa vifaa vya mazoezi katika Klabu ya Gofu ya Lugalo ili kuhakikisha kila siku za mwisho wa wiki vijana sasa wanapata mafunzo bure. Katika hatua nyingine, Mziray alisema kama Benki imekuwa ikisimama kuhakikisha kila mwenye ndoto anaweza kuzitimiza kulingana na mipango waliyonayo.