Moshi, Kilimanjaro – 21 Machi 2026. Yas imeendelea kusukuma mbele juhudi za uhifadhi wa mazingira kupitia kampeni ya Yas Green for Kili, ikiwa na lengo la kulinda vyanzo vya maji, kurejesha uoto wa asili na kuimarisha mazingira ya Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza na wananchi, wadau wa uhifadhi na washiriki wa tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kulinda rasilimali za asili za mkoa huo.
“Mpango huu wa Yas unaonyesha wazi namna sekta binafsi inavyoweza kuchukua nafasi ya msingi kwenye kulinda mazingira. Kupanda miti, kuhamasisha jamii na kulinda vyanzo vya maji kunaleta faida ambazo wananchi wanaanza kuziona katika maisha ya kila siku. Kama mkoa, tutaendelea kuwa bega kwa bega na wadau wote wanaochukua hatua kwa vitendo,” alisema Mhe. Babu.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas, Pierre Canton Bacara, alisema kampeni hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2021 – imekuwa na matokeo ya kweli kutokana na ushirikiano wa karibu na Serikali, wadau wa uhifadhi na wakazi wa maeneo yanayozunguka hifadhi. Zaidi ya miti 96,000 imepandwa, huku kiwango cha uhai wa miche kikiwa juu zaidi ya asilimia 95.
“Hatuna mafanikio ya kudumu bila ushirikiano. Tumepiga hatua kubwa kwa sababu jamii imekuwa sehemu ya safari hii. Tunachokifanya hapa si kazi ya msimu, ni kazi ya kujenga mustakabali wa vyanzo vya maji na misitu ya eneo hili,” alisema Bacara.
Mwaka huu, Yas imeongeza nguvu kwa kufanya kampeni za uhamasishaji shuleni, usafi kwenye vyanzo vya maji na hatua nyingine za kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa matumizi endelevu ya rasilimali. Kupitia tukio la leo, kampuni imepanda miche 3,000 ikiwa sehemu ya lengo la miti 50,000 litakalotekelezwa mwaka 2026.
Bacara aliongeza kuwa dhamira ya Yas haiko tu kwenye huduma za mawasiliano, bali pia kwenye kulinda mazingira yanayowawezesha Watanzania kuishi na kufanya kazi zao kwa furaha na amani. Alipongeza ushirikiano wa Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro, taasisi za uhifadhi (KINAPA, TFS, Bonde la Mto Pangani) na wananchi wote walioungana katika kampeni hiyo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas, Pierre Canton Bacara, akipanda mti wakati wa kampeni ya mazingira ya “YAS Go Green for Kili” iliyofanyika hivi karibuni mjini Moshi. Yas Green for Kili ni sehemu ya dhamira endelevu ya kampuni katika kulinda mfumo wa ikolojia wa Mlima Kilimanjaro, kuhifadhi vyanzo muhimu vya maji pamoja na kuimarisha ushirikiano na wadau pamoja na jamii kwa ujumla katika juhudi za uhifadhi.