Baba mdogo, mjumbe waibua mapya mauaji ya Linah

Dar es Salaam. Wakati mjumbe wa shina namba sita wa Tawi la Mkwajuni Kata ya Vijibweni, Kigamboni, Aloyce Msiagi akieleza namna mtuhumiwa wa mauaji ya Linah Kabamba alivyomburuza dada yake kutoka koridoni alikofanyia mauaji hadi chumbani, baba mdogo wa marehemu amesema marehemu alimchukua mdogo wake huyo na kuishi naye akimfundisha kazi.

Linah ambaye ni mama wa watoto wanne na mke wa Chriss Kabamba, aliyefunga naye ndoa mwezi mmoja uliopita, alipoteza maisha kwa kuchomwa kisu, saa 7 mchana wa Machi 20, 2026 nyumbani kwao, Rynes, Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ameijuza Mwananchi kuwa tukio hilo lipo na tayari mtuhumiwa amekamatwa na upelelezi unaendelea kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Leo Jumanne, Machi 24, 2026, Mwananchi limefika msibani Kigamboni ambapo taratibu za mazishi zinaendelea na kupata fursa ya kuzungumza na Herman Elinewinga, ambaye ni baba mdogo wa marehemu pamoja na mjumbe wa shina namba tisa, Aloyce Msiagi.

Mwili wa Linah umechukuliwa leo Jumanne, saa 11 jioni kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni ulikokuwa umehifadhiwa na kupelekwa nyumbani hapo na kesho Jumatano saa 7 mchana utaagwa katika ibada itakayofanyika Kanisa la Luthelani Kisiwani kwa ajili ya maziko yatakayofanyika makaburi ya Kisota Kigamboni.

Katika maelezo yake, Elinewinga amedai Linah alichomwa kisu na mdogo wake wa pili kutoka mwisho kuzaliwa, aliyemtaja kwa jina la Meshack.

Mume wa Lina, Chris Kabamba (mwenye shati ya kijani ya jeshi) akiwa na waombolezaji wengine.

Amesema Linah aliyezaliwa mwaka 1990 ni mtoto wa kwanza na  ana wadogo zake saba, ambao wawili alikuwa akiishi nao hapo nyumbani, ambao ni Lightness na Meshack wanaofuatana kuzaliwa.

“Meshack (mtuhumiwa) aliishi naye hapa akimfundisha mambo ya biashara, akimtuma,” amesema baba mdogo wa marehemu na kufafanua.

“Meshack alikuja Dar muda mrefu kidogo, hivi karibuni ndipo alianza kukaa na dada yake akiwa anamuelekeza ili naye aingie kwenye mfumo wa biashara kama yeye (Linah).”

Amesema siku ya tukio, watoto wa Linah hawakuwepo nyumbani, walikwenda kwa baba yao mdogo kwa kuwa ilikuwa ni kipindi cha sikukuu ya Idd.

“Linah ana watoto wanne, mkubwa ana miaka 16 na mdogo miaka mitatu, hawakuwepo nyumbani siku ya tukio,” amesema.

Anasema siku hiyo nyumbani alikuwepo Linah, wadogo zake wawili na mama mkwe wake huku mumewe (Chris Kabamba) akiwa kwenye biashara zake Kariakoo.

Alipoulizwa kuhusu chanzo cha mauaji hayo na kama ni kweli kulikuwa na mzozo wa wadogo zake marehemu, Herman amesema si kweli.

Ingawa awali majirani na mume wa marehemu walieleza kuwepo kwa mzozo huo na Linah alitoka kuingilia ndipo akachomwa kisu na kupelekea mauti.

Baba yao mdogo amesema taarifa hizo si za kweli kutokana na jinsi walivyoishi hapo nyumbani kama watoto wa baba mmoja.

“Mimi siishi hapa nilipata taarifa kama wengine, ingawa si kweli kwamba kulikuwa na mzozo, ili jambo lipo polisi wao ndio watatupa taarifa zaidi,” amesema.

Kuhusu mtuhumiwa kuwa na matatizo ya akili, baba mdogo huyo amesema hawezi kuthibitisha hadi ripoti ya madaktari.

Amesema kama familia kwa sasa wanashughulikia taratibu za mazishi na baada ya hapo ndipo masuala mengine ya kipolisi yataendelea.

“Tunahitaji tumalize mazishi kwanza kisha tusikilize polisi wanasemaje kuhusu hilo, hivi sasa tumekamilisha taratibu za kipolisi za kuchukua mwili,” amesema.

Jana Jumatatu, Chris Kabamba ambaye ni mme wa Lina akisimulia tukio hilo alipozungumza na Mwananchi alisema shemeji zake hao wawili, walikuwa katikati ya mzozo, uliosababisha mkewe akaingilie kati kuamulia, aliishia kuchomwa visu na kupoteza maisha.

“Siku hiyo nyumbani alikuwepo mama yangu (mkwewe Lina) na mdogo wake na Lina wa kike ambaye ndiye alipiga kelele kuomba msaada kwa majirani baada ya mdogo wao mwingine kufanya mauaji hayo,” anasema.

Katika mitandao ya kijamii, alisema inapotoshwa kuwa aliyemchoma kisu Linah ana matatizo ya akili, lakini uhalisia ni kijana mwenye umri wa miaka 19 na ni shemeji yake na hana tatizo la afya ya akili kama inavyodaiwa.

“Ana akili timamu, ulitokea mzozo hapa nyumbani, yeye na ndugu yake mwingine, mke wangu akaingia kuamulia, ndipo likatokea hilo lililotokea. Taarifa zaidi mkitaka mtapewa na OCD wa Kigamboni ndiye anafuatilia suala hili,” anasema Kabamba.

Mwananchi limezungumza na Msiagi ambaye ni mjumbe wa shina namba tisa ambaye amesema alipigiwa simu na jirani wa Linah kutaka afike eneo la tukio.

Amesema alifika na kukuta damu nyingi zimetapakaa chumbani kwa marehemu na mwili wa Linah ukiwa sakafuni.

“Ndugu walitaka wambebe kumpeleka hospitali, lakini nilipomuangalia, tayari alikuwa amepoteza maisha, nilifanya mawasiliano na polisi, walifika na watu wa afya walipompima wakakuta tayari amefariki,” amedai.

Amesema alipofika eneo la tukio, alikuta mtuhumiwa anataka kukimbia na kushirikiana na watu wengine kumfunga kamba wakati huo wakisubiri polisi.

Amesema walikuta kisu alichokitumia kikiwa chumbani kwa marehemu kitandani na fulana aliyokuwa amevaa mtuhumiwa ikiwa huko.

Waombolezaji wakiwa msibani.

“Alimuulia kwenye korido, akamburuza hadi chumbani, pale koridoni akapadeki pakawa hakuna damu,” amedai.

Amesema siku hiyo nyumbani kulikuwa watu wanne na kwa mujibu wa maelezo ambayo yeye mjumbe alipewa na mdogo wa marehemu wa kike, mtuhumiwa alimfuata binti huyo jikoni akiwa ameshika kisu.

“Yule binti alikimbilia chumbani na kufunga mlango, mtuhumiwa akawa anagonga kwa nguvu, ndipo Linah akatoka chumbani kwake kwenda kuangalia kuna nini, ndipo akakutana na mtuhumiwa koridoni akamchoma,” amedai.

Amesema walivyokuta mtuhumiwa ni kama marehemu naye alikuwa akipambana kujitetea kwani alikuwa na alama za kung’atwa mikononi na marehemu alikuwa na majeraha shingoni, tumboni na sehemu nyingine za mwili.

“Yule mtuhumiwa baada ya kufika askari walimuuliza akawa anaongea vitu havieleweki, alisema mara Linah alimtumia watu wanataka kumuua, mara alimtukana, wakamuhoji ndiyo umuue? Hakukuwa na maelezo kamili,” amesema.