Chadema ni suala la muda kama ‘ndiyo’ au hapana

Dodoma. Hatima ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuendelea kuzuiwa kufanya shughuli za kisiasa au kurejea ulingoni sasa ipo mikononi mwa Mahakama ya Rufaa, baada ya zaidi ya siku 283 tangu kilipowekewa zuio hilo.

Hadi sasa, bado haijafahamika ni lini uamuzi wa mwisho utatolewa, huku jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, Mwarija Agostino, Issa Maige na Abraham Mwampashi, likisubiri kukamilisha uandishi wa hukumu baada ya kusikiliza hoja za pande zote.

Shauri hilo limesikilizwa leo Jumanne Machi 24, 2026, katika Mahakama ya Rufaa Dodoma na kuhudhuriwa na wanachama wengi wa Chadema waliovalia sare za chama hicho, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake Bara, John Heche.

Chadema ilifikisha shauri hilo mahakamani hapo ikiomba marejeo ya uamuzi wa Mahakama Kuu uliosababisha kuzuiwa kwa shughuli zake za kisiasa pamoja na matumizi ya mali za chama hicho.

Awali, katika kesi ya msingi namba 832/2025 iliyofunguliwa na Saidi Mohamed na wenzake dhidi ya Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa chama hicho, Mahakama Kuu ilitoa amri ya zuio Juni 10, 2025 kupitia Jaji Mwanga, hatua iliyosababisha chama hicho kusimamishwa shughuli zake.

Katika kesi hiyo, walalamikaji walipinga matumizi ya mali za chama, majengo pamoja na uendeshaji wa shughuli za kisiasa, wakidai kuwepo kwa ukiukwaji wa taratibu na masilahi yao.

Viongozi wa Chadema wakizungumza na Mawakili wao muda mfupi baada ya kesi yao kusikilizwa katika mahakama ya Rufaa Jijini Dodoma.

Kesi ya marejeo katika Mahakama ya Rufaa imepewa namba 1/2026 pamoja na Civil Revision namba 2/2026, 3/2026 na 4/2026, huku upande wa Chadema ukiwakilishwa na jopo la mawakili akiwemo Rugemeleza Nshala, Mpale Mpoki, Gaston Garubimbi, Dickson Matata, Mwashipu Hekima na Nashon Nkungu.

Usikilizwaji wa shauri hilo ulianza saa 3:30 asubuhi hadi saa 7:00 mchana, kabla ya kuendelea tena saa 8:05 mchana hadi saa 10:52 jioni.

Akiahirisha kesi hiyo, Jaji Kiongozi Mwarija Agostino amesema Mahakama imekamilisha kusikiliza hoja zote na sasa inahitaji muda wa kuandika hukumu, huku tarehe ya uamuzi ikitarajiwa kutangazwa na msajili wa Mahakama.

“Ndugu mawakili wa pande zote, tunawashukuru kwa hoja zenu. Tumezisikiliza na tunaomba muda wa kuandaa hukumu. Mtajulishwa tarehe ya kuja kusikiliza uamuzi,” amesema.

Akizungumza nje ya Mahakama, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Rugemeleza Nshala amesema hoja kuu zilizokuwa na mvutano wa kisheria ni pamoja na mwanzo wa mgogoro huo, thamani ya mali zinazobishaniwa, iwapo katiba ya chama ilizingatia masilahi ya pande zote, pamoja na uhalali wa baadhi ya wajumbe wa bodi kuwa wadai.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema wana imani kuwa haki itatendeka, akieleza kuwa hatua ya mahakama kuagiza mafaili yote ya kesi kuwasilishwa ni ishara ya msingi mzuri wa haki.

Kwa upande wa walalamikaji, Wakili Shaban Marijani amesisitiza kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu ulikuwa sahihi, wana imani  Mahakama ya Rufaa nayo itatenda haki.

Viongozi wengine waliohudhuria kesi hiyo ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu Bara, Aman Golugwa.

Tofauti na ilivyozoeleka katika kesi nyingine za Chadema, safari hii hakukuwa na ulinzi mkali nje ya mahakama, huku askari wachache wameonekana katika eneo hilo.

Ndani ya ukumbi wa mahakama, hali ilikuwa ya kipekee kwani kulikuwa na vicheko na kejeli za hapa na pale wakati wa hoja za mawakili, hali iliyoonyesha namna kesi hiyo ilivyokuwa na mvuto kwa wasikilizaji.

Viongozi wa Chadema wakizungumza na Mawakili wao muda mfupi baada ya kesi yao kusikilizwa katika mahakama ya Rufaa Jijini Dodoma.

Aidha, Rugemeleza Nshala hoja yake naye ilizua kicheko aliposema kuwa kazi ya uwakili wakati mwingine inaweza kusababisha mtu kupata msongo wa mawazo iwapo hatakuwa makini.

Akijibu kwa utani, Jaji Mwarija Agostino alimkumbusha kuwasilisha hoja zake kwa utulivu ili kuepuka athari za kiafya.