Familia ya Nyanza yaendelea kusubiri mwili wauzike, yahofia gharama

Dar es Salaam. Huzuni imeendelea kuitawala familia ya Athumani Nyanza, anayedaiwa kuuawa na kufukiwa mbele ya nyumba yake kabla ya kubainika na kufukuliwa, baada ya kupita siku kadhaa bila nduguze kukabidhiwa mwili kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Zimeshapita siku nane, tangu familia ilipoweka msiba Chanika, jijini Dar es Salaam, baada ya kubaini na kuufukua mwili wa marehemu. Hata vifaa vilivyokodishwa ikiwemo viti na maturubai, vimeisha muda wake na vimerudishwa kwa wenyewe.

Idadi hiyo ya siku zilizoyoyoma bila familia kupewa mwili, imesababisha msiba usiishe nyumbani hapo, huku waombolezaji wakisambaratika na sasa wamebaki ndugu wa karibu pekee.

Kifo cha Nyanza kilibainika baada ya mwili wake kudaiwa kufukiwa kwenye shimo mbele ya nyumba yake iliyopo katika mtaa huo na baadaye kufukuliwa Machi 16, 2026, hali iliyozua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza na Mwananchi, leo Machi 24, 2026 baba mdogo wa marehemu, Omari Nyanza, amesema pamoja na hali hiyo, familia imeendelea kufuatilia suala hilo katika vyombo vya dola.

“Tunaendelea kwenda polisi mara kwa mara kufuatilia mwili wa mpendwa wetu, lakini tunaelezwa tusubiri majibu kutoka kwa mkemia mkuu. Wanasema wanataka kuhakikisha utambuzi wa mwili unakuwa sahihi ili kusiwe na kasoro hata ndogo katika uendeshaji wa kesi,” amesema Nyanza.

Amesema Jeshi la Polisi limewaambia sampuli zilizochukuliwa zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya vipimo vya vinasaba (DNA).

“Tuliambiwa majibu tutapewa baada ya saa 24 hadi 48 lakini tumeendelea kusubiri hadi leo ambayo inatimia siku ya nane tangu mwili kufukuliwa,” amesema Nyanza.

Amesema wamekuwa wakifuatilia upatikanaji wa mwili wa ndugu yao hata kwa kumtumia Madebe Lidai ambaye ni rafiki wa Athumani.

Amesema licha ya uelewa huo, hali ya kusubiri imeendelea kuwaumiza zaidi ndugu, ambao tayari walishauona mwili huo baada ya kufukuliwa lakini changamoto kubwa ni kukabidhiwa ili wauzike.

Pia, amesema wanapata wasiwasi wa kuhifadhi mwili mochwari kwani gharama kwa siku ni Sh30,000 hivyo wana hofu endapo wataambiwa wanahitaji kulipia.

“Hali hii pia inatupa mashaka kwenye gharama ya kulipia maiti mochwari tunafahamu kuhifadhi kwa siku moja ni Sh30,000 kwa siku zote alizokaa ndugu yetu tunaogopa itakuja gharama kubwa endapo tutaambiwa tulipie, kama italipiwa na Serikali sawa lakini wenyewe tutajikuta tuna mzigo mkubwa,”amesema.

Hata hivyo, amesema kuchelewa kwa majibu hayo kumeathiri mwenendo mzima wa msiba, huku ndugu wakilazimika kubadili mipango yao mara kwa mara.

Mbali na hilo, ndugu wameendelea kukumbwa na changamoto za kifedha na kisaikolojia, wakieleza kuwa hali ya kusubiri bila majibu imeongeza maumivu zaidi.

Pia, Omari amesema kwa mujibu wa imani ya dini ya Kiislamu, marehemu anapaswa kuzikwa haraka, jambo ambalo limekuwa haliwezekani kutokana na kusubiri matokeo hayo.

“Kwa imani yetu, haipaswi kupita muda mrefu hivi bila mazishi, sasa imekaribia wiki nzima tangu mwili kupatikana na sisi hatuwezi kusema tuna mwili kwa sababu hatujakabidhiwa, hivyo tunaendelea kusubiri,” amesema.

Amesema familia ipo tayari kuuzika mwili huo mara tu watakapokabidhiwa, wakipanga kusafirisha kwenda kijijini Chole, Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani kwa mazishi rasmi ya kifamilia.

Akizungumza jana Machi 23, 2026 Neema Lusekelo, jirani wa marehemu alisema kuna haja ya ndugu kukabidhiwa mwili ili wamalize msiba kwani wamekuwa wakihangaika kupata mwili wa ndugu yao.

“Kama walipewa siku mbili hadi tatu na sasa ni wiki wanapima vitu gani vingine na watuhumiwa wapo ndani wanawaumiza ndugu na mtoto wake maana hajui baba yake atazikwa lini na hapo ni kufufua msiba upya,”amesema Neema.

Amesema ndugu wamejikuta wanaongeza gharama za kulipia vitu na kuchangishana kila siku kwa sababu hawajui watapewa lini mpendwa wao huku wakiendelea kukaa na vitu vya watu ikiwepo maturubai na viti ambavyo vyote vinalipiwa kwa siku.