Gamondi ataja mawili Stars ikienda Rwanda

KOCHA wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Miguel Gamondi amesema kikosi chake kipo katika maandalizi mazuri kuelekea mashindano ya FIFA Series, akisisitiza lengo kuu ni kujenga timu yenye ushindani na uwezo wa kufanya vizuri.

Taifa Stars itatupa karata yake ya kwanza huko Rwanda, Machi 26 mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Liechtenstein. Baada ya kukabiliana na timu hiyo kutoka Ulaya, itakuwa na mechi nyingine lakini itategemea na matokeo katika mechi yake ya kwanza.

Kama vijana hao wa Gamondi wataichapa Liechtenstein, basi watacheza fainali Machi 29 mwaka huu na mshindi kati ya Aruba kutoka Amerika au Macau kutoka Asia na kama itapoteza basi itacheza mechi ya mshindi wa tatu na aliyepoteza mechi ya pili baina ya timu hizo.

Kikosi hicho kilichoingia kambini Jumapili ya Machi 22 mwaka huu, leo Jumanne kimeondoka Dar es Salaam kuelekea Rwanda kwa ajili ya mashindano hayo.

Akizungumza kuhusu hatua za awali za maandalizi, Gamondi amesema: “Tumeanza maandalizi kwa umakini mkubwa, tukijenga msingi imara wa timu.”

Kocha huyo alifafanua kuwa maandalizi hayo yanahusisha mambo mengi ikiwemo mbinu za kiufundi, nidhamu ya wachezaji pamoja na kuimarisha mshikamano wa kikosi, ambacho ni muhimu katika mashindano ya aina hiyo.

Alikiri kuwa mchakato wa kuchagua kikosi ulikuwa na changamoto, akisema:

“Tumelazimika kufanya maamuzi magumu mara kwa mara ili kupata kikosi sahihi kitakachoiwakilisha nchi.”

Gamondi aliongeza kuwa licha ya changamoto hizo, ana imani kubwa na wachezaji alio nao, akibainisha kuwa kila mmoja ana uwezo na dhamira ya kuitumikia timu ya taifa kwa kiwango cha juu.

Akizungumzia ushindani ndani ya kikosi, amesema kuwa hali hiyo ni chanya kwa maendeleo ya timu, kwani inawafanya wachezaji kujituma zaidi ili kupata nafasi ya kucheza.

Pia alieleza kuwa bado kuna maeneo yanahitaji maboresho, lakini benchi la ufundi linaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha timu inakuwa katika hali bora kabla ya kuanza kwa michuano hiyo.

FIFA Series 2026, ni toleo la pili la mashindano hayo yanayoandaliwa na FIFA ambayo yanaangazia mechi za kirafiki kati ya timu za taifa kutoka mashirikisho tofauti ya bara.

Toleo hili litaangazia makundi tisa yaliyogawanywa kwa timu nne unaofanyika katika nchi nane zilizopewa uwenyeji kuanzia Machi 25 hadi 31 mwaka huu.

Tanzania kituo chake ni Rwanda ikitumia Uwanja wa Kigali Pele ambapo ipo na nchi za Aruba, Liechtenstein na Macau, huku mechi zikichezwa Machi 26 na 29. Awali ilipangwa kwenda Mauritius, lakini ikahamishiwa Rwanda baada ya nchi hiyo kujiondoa katika nafasi ya kuwa mwenyeji.