IHI yatafiti kipimo cha ulimi kubaini kifua kikuu

Dar es Salaam. Utafiti mpya wa Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) umeibua matumaini ya kurahisisha utambuzi wa vimelea vya kifua kikuu kwa kutumia mbinu mbadala ya usufi wa ulimi badala ya makohozi.

Njia hiyo mbadala ya kugundua TB, ambayo inaweza kuwa nyepesi, haraka na rahisi kwa wagonjwa, imebainishwa leo Jumanne, Machi 24, 2026 wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kifua kikuu Duniani.

Kwa muda mrefu vipimo vya TB vimekuwa vikitegemea makohozi, lakini sasa taasisi hiyo inaangalia mbinu ya kutumia usufi wa ulimi (tongue swab) kuchunguza vinasaba vya bakteria wa TB.

Hii ni hatua ambayo inaweza kuboresha utambuzi hasa kwa watoto na wagonjwa wa Virusi vya Ukimwi (VVU) ambao mara nyingi hushindwa kutoa makohozi ya kutosha.

Akizungumza na Mwananchi leo Machi 24, 2026, Mtaalamu wa mikrobiolojia na mchambuzi wa utafiti wa kitabibu, Hellen Hiza amesema njia hii inaweza kuokoa muda na kurahisisha upatikanaji wa vipimo vya TB.

“Watumiaji hawanunuliwi vipimo vingine kwa gharama za ziada, na wagonjwa hawawezi kuchelewa kugundulika au kuanza matibabu,” amesema Hiza.

Mbinu hii pia inachunguza uwezekano wa kutumia damu kidogo badala ya makohozi, jambo linaloweza kusaidia kugundua ugonjwa huo mapema na kufuatilia maendeleo ya wagonjwa wakiwa nyumbani.

Kupitia teknolojia hiyo, watafiti wanachunguza pia vinasaba vya bakteria wa TB ili kubaini kama kuna usugu wa dawa, jambo linalosaidia madaktari kuchagua matibabu sahihi mapema.

IHI pia inatafiti kugundua TB isiyo na dalili, ambapo mtu anaweza kuambukiza wengine bila kujua, hatua ambayo ikifanikiwa inaweza kupunguza maambukizi katika jamii.

Hii ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha huduma za kifua kikuu zilizosogezwa karibu na wagonjwa, kupunguza gharama za usafiri na kuimarisha ufanisi wa matibabu.

Kila mwaka, watu milioni 2.4 duniani hawagunduliwi wala hawaripotiwi kuwa na kifua kikuu, hali inayoongeza hatari ya maambukizi na madhara makubwa kiafya.

Hiza amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali, pamoja na kuendeleza utafiti wa ndani katika vipimo, dawa na chanjo, ni muhimu katika vita dhidi ya kifua kikuu.

“Tukibadilisha mtazamo na kuweka wagonjwa mbele ya huduma, si tu tunarahisisha upatikanaji wa matibabu, bali pia tunaokoa maisha,” amesema.

Hiza, amesema licha ya matibabu ya TB kutolewa bure, wagonjwa wengi wanakumbana na vikwazo vinavyochelewesha utambuzi na matibabu.

Ametaja changamoto zinazowakwanza, kuwa ni pamoja na umbali mrefu wa kufuata huduma, gharama za usafiri na muda mrefu wa kusubiri huduma, hivyo wengi kuchelewa kugundulika au kushindwa kukamilisha matibabu.

“Ni muhimu kusogeza huduma karibu na wananchi. Teknolojia kama matumizi ya simu inaweza kusaidia kupunguza muda wa kusubiri majibu na kufuatilia wagonjwa wakiwa nyumbani, hivyo kupunguza upotevu wa wagonjwa katika mfumo wa matibabu,” amesema Hiza.

Amesisitiza pia umuhimu wa kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kusambaza dawa na kufuatilia wagonjwa au kutumia ujumbe mfupi wa simu kuhakikisha wanakamilisha dozi kwa wakati, badala ya kuwalazimisha wagonjwa kusafiri umbali mrefu.

Hata hivyo, Hiza amebainisha kuwa Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, haiwezi kufanya kazi hiyo peke yake, hivyo kuna haja ya kushirikisha sekta binafsi katika uchunguzi, utambuzi, matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa.

“Ushirikishwaji wa sekta binafsi utapunguza mzigo kwa Serikali na kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya TB,” amesema.

Hiza amesema mafanikio ya mapambano dhidi ya kifua kikuu yanategemea pia uwekezaji katika tafiti za ndani, maendeleo ya vipimo, dawa na chanjo.

Amesema kuna haja ya kubuni mbinu mbalimbali za ufadhili ili kuunga mkono ubunifu wa ndani kwa lengo la kuboresha afya za Watanzania.

Kwa ujumla, ameeleza kuwa kuweka mgonjwa katikati ya huduma, si tu kunarahisisha upatikanaji wa matibabu, bali pia kunachangia kuokoa maisha na kupunguza maambukizi katika jamii.

“Uchunguzi wa Watanzania kwa ajili ya kuboresha afya ni muhimu katika kufikia malengo ya kutokomeza kifua kikuu,” amesema.