KAMATI YA BUNGE UWEKEZAJI MITAJI YA UMMA YARIDHISWA NA MRADI WA MAKAZI WA CANADIAN MASAKI

 


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Masanja Kadogosa, leo Machi 24, 2026 ameongoza ziara ya ukaguzi wa mradi wa Canadian Village Awamu ya Kwanza uliopo wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Mradi huo unaotekelezwa katika eneo lenye ukubwa wa takribani ekari 6.4, ni miongoni mwa miradi inayolenga kukuza uwekezaji wa mitaji ya umma na kuboresha miundombinu ya makazi ya kisasa.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Kadogosa alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi ya aina hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha, ubora wa kazi, pamoja na kukamilika kwa wakati ili kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa. Alieleza kuwa kamati itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya uwekezaji wa umma nchini.

Kwa upande wake, Naibu anayehusika na masuala ya ujenzi, Mhe. Msonde, alieleza kuwa maendeleo ya mradi huo yanaendelea vizuri, huku akibainisha kuwa jitihada zinafanyika kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa wakati ili kuepusha ucheleweshaji.

Aidha, aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha mazingira ya makazi pamoja na kuongeza thamani ya uwekezaji katika eneo hilo.

Ziara hiyo ni sehemu ya jukumu la Kamati ya PIC kuhakikisha kuwa uwekezaji wa mitaji ya umma unaleta tija, unazingatia uwajibikaji, na unachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.