KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MIRADI YA TBA MASAKI

              *******

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kufuatia ziara ya kukagua nyumba za makazi zilizojengwa eneo la Masaki, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Masanja Kadogosa, amesema majengo hayo yanaonesha thamani ya fedha iliyowekezwa, akibainisha kuwa kila jengo linakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 4.6.

Amesema pia kila jengo lina uwezo wa kuchukua familia 12, hali inayochangia kupunguza changamoto ya makazi katika maeneo ya mijini.

Kadogosa alieleza kuwa kamati imejiridhisha kuwa miradi hiyo inatekeleza kwa vitendo ilani ya Chama Cha Mapinduzi, hasa katika kuboresha upatikanaji wa nyumba bora kwa wananchi.


Aidha, ameipongeza TBA kwa kutumia mbinu bunifu za utekelezaji wa miradi, ikiwemo mfumo unaoruhusu matumizi ya mikopo, hatua inayosaidia kupunguza utegemezi wa fedha za serikali.

Kamati hiyo pia imeitaka TBA kuendeleza awamu nyingine ya ujenzi itakayoanza mwaka ujao wa fedha ili kuongeza idadi ya nyumba na kukidhi mahitaji yanayoongezeka.


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Charles Msonde, amesema serikali imepanga kujenga zaidi ya majengo 18 katika eneo hilo kupitia TBA.

Amesema hadi sasa majengo matatu yamekamilika na tayari yanahudumia familia 36, huku wakazi wote wakiwa wamepangiwa.

Msonde alibainisha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unategemea mapato ya ndani ya TBA, jambo linalosaidia kupunguza mzigo kwa serikali.

Aidha, amesema mabadiliko ya sheria ya mwaka 2003 yameiwezesha TBA kutumia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), hatua inayoongeza kasi ya ujenzi wa makazi bora nchini.