KUTOKA AKIBA HADI UWEKEZAJI: Safari ya mwanamke wa Kitanzania kwenye uchumi rasmi

Dar es Salaam. Katika muktadha wa mabadiliko ya kiuchumi yanayoendelea kushika kasi duniani, nafasi ya mwanamke wa Kitanzania katika uzalishaji wa utajiri imeanza kuchukua sura mpya.

Siyo tena zama za kutegemea akiba kama njia pekee ya kujihakikishia usalama wa kifedha, bali ni wakati wa kukumbatia mifumo rasmi ya uwekezaji, benki na hifadhi ya jamii ili kujenga msingi imara wa maisha ya baadaye.

Mwelekeo huo ulijitokeza wazi wakati wa mjadala wa makongamano tofauti kwenye The Citizen Rising Woman 2026, yaliyoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communication Limited, ambayo kilele chake kilifanyika Machi 8, 2026, ambapo wataalamu wa masuala ya fedha, masoko ya mitaji, benki na mifuko ya hifadhi ya jamii walikutana na kujadili namna bora ya kumwezesha mwanamke kiuchumi.

Kaulimbiu ya kongamano hilo ilikuwa ni: “Wanawake katika uzalishaji wa utajiri: Kutoka akiba hadi uwekezaji na ukuaji wa biashara,” likibeba ujumbe mzito unaolenga kubadili fikra na mtazamo wa wanawake wengi nchini.

Kwa muda mrefu, akiba imekuwa ikionekana kama nguzo kuu ya nidhamu ya kifedha kwa wanawake. Hata hivyo, wataalamu wanaeleza kuwa ingawa akiba ni muhimu, haitoshi peke yake kujenga utajiri wa kudumu.

Dalali wa dhamana, Stella Riwa, anabainisha kuwa uundaji wa utajiri ni mchakato wa muda mrefu unaohitaji zaidi ya kuhifadhi fedha.

 Anasema uwekezaji ndiyo hatua inayofuata baada ya akiba na kwamba wanawake wanapaswa kuanza mapema ili kunufaika na faida ya riba mchanganyiko, ambayo huongeza thamani ya fedha kadri muda unavyopita.

Kwa mujibu wa Riwa, muda ni silaha muhimu kwa mwekezaji, na kuchelewa kuanza kunaweza kupunguza fursa ya kukuza mtaji.

Hata hivyo, anaonya kuwa uwekezaji unahitaji uelewa wa kina. Kabla ya kuwekeza katika kampuni au chombo chochote cha kifedha, ni lazima mwekezaji afanye uchambuzi wa kina kuhusu utendaji wa kampuni husika, atathmini hatari zinazoweza kujitokeza na, inapobidi, kushauriana na wataalamu wenye leseni.

Anasisitiza kuwa uwekezaji si kamari, bali ni mkakati unaohitaji nidhamu na udhibiti wa hisia, hasa katika mazingira ambapo bei za hisa hupanda na kushuka.

Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mecklaud Edson, anasisitiza kuwa uwekezaji una nafasi kubwa katika kuwawezesha wanawake kumiliki mali.

Anasema tofauti na akiba, ambayo hulinda fedha, uwekezaji huipa fedha uwezo wa kuzalisha thamani zaidi.

Edson anaeleza kuwa kupitia soko la hisa, wanawake wanaweza kununua hisa na kuwa wanahisa katika kampuni mbalimbali, hatua inayowawezesha kumiliki sehemu ya uchumi wa nchi. Kadri kampuni hizo zinavyokua, ndivyo thamani ya uwekezaji wao inavyoongezeka.

Anataja fursa mbalimbali zilizopo katika DSE, zikiwamo hati fungani za Serikali zinazotoa mapato yenye uhakika kwa kipindi maalumu, hati fungani za kampuni zinazoweza kutoa kipato cha mara kwa mara, pamoja na mifuko ya uwekezaji inayouzwa sokoni (ETFs).

 Mifuko hiyo, kwa mujibu wake, huwapa wawekezaji nafasi ya kugawanya uwekezaji wao katika maeneo mbalimbali kwa wakati mmoja, hivyo kupunguza hatari.

Edson pia anasisitiza kuwa uwekezaji hauhitaji mtaji mkubwa kuanza, akibainisha kuwa hata vikundi vya kijamii kama vikoba na Saccos vinaweza kutumia mifumo rasmi kuingia katika uwekezaji wa masoko ya mitaji na hivyo kuongeza kipato cha wanachama wao.

Katika kuonesha mabadiliko ya nafasi ya mwanamke katika uchumi, Edson anatoa mfano wa Benki ya NMB akieleza kuwa inaongozwa na mwanamke, jambo linalodhihirisha kuwa wanawake wanaweza kuwa viongozi wakuu katika taasisi kubwa za kifedha.

Mbali na uwekezaji, wataalamu wanasisitiza umuhimu wa urasimishaji wa biashara kupitia huduma za benki. Mkuu wa Bidhaa na Njia za Huduma wa Absa Bank Tanzania, Jane Kalumuna, anasema biashara nyingi zinazoendeshwa na wanawake bado haziko katika mfumo rasmi wa kifedha, hali inayozuia upatikanaji wa mikopo na huduma nyingine muhimu.

Kalumuna anasema kuwa na akaunti ya benki ni hatua muhimu katika kujenga uaminifu wa kifedha. Kupitia akaunti hiyo, mjasiriamali anaweza kuonesha mzunguko wa fedha katika biashara yake, jambo linalosaidia taasisi za kifedha kutathmini uwezo wake wa kukopa.

Anabainisha kuwa akaunti maalumu za biashara, kama SHE Business zinazotolewa na benki hiyo, zinalenga kuwawezesha wanawake katika sekta ya biashara ndogo na za kati kwa kuwapatia huduma zinazokidhi mahitaji yao.

Kwa mujibu wake, uhusiano rasmi na benki husaidia kufanya uamuzi sahihi wa kifedha na kuchochea ukuaji endelevu wa biashara. Suala la hifadhi ya jamii limeendelea kupewa uzito kama sehemu muhimu ya usalama wa kifedha wa muda mrefu.

Meneja wa Sekta Isiyo Rasmi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Rehema Chuma, anasema wanawake wengi, hasa waliopo katika sekta isiyo rasmi, hawana mipango madhubuti ya kustaafu.

Anatahadharisha kuwa hali hiyo inaweza kuwaweka katika mazingira magumu wanapokumbwa na changamoto za maisha kama magonjwa, ulemavu au kupoteza kipato.

Kwa mujibu wake, kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ni hatua muhimu ya kujikinga dhidi ya hatari hizo.

Chuma anasema kupitia NSSF, wanachama hupata faida mbalimbali zikiwamo fidia ya uzeeni, ulinzi dhidi ya majanga, pamoja na faida ya uzazi kwa wanawake. Anasisitiza kuwa michango ya leo ndiyo msingi wa kipato cha kesho, akibainisha kuwa uzee ni hatua isiyokwepeka katika maisha ya binadamu.

Kwa ujumla, mjadala wa wataalamu unaonesha kuwa safari ya mwanamke kuelekea kujenga utajiri inahitaji mkakati mpana unaojumuisha uwekezaji, urasimishaji wa biashara na hifadhi ya jamii.

Mifumo hiyo mitatu kwa pamoja ina uwezo wa kumwezesha mwanamke kujenga uchumi wake kwa njia endelevu.

Ujumbe unaojitokeza ni kwamba fursa za kifedha zipo na zinapatikana kwa urahisi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Hata hivyo, kinachohitajika ni mabadiliko ya mtazamo, kuacha kutegemea akiba pekee na kuchukua hatua za kuingia katika uwekezaji na mifumo rasmi ya kifedha.

Kwa mwanamke wa Kitanzania, hii si tu fursa ya kuboresha maisha yake binafsi, bali pia ni mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla. Kadri wanawake wanavyoongeza ushiriki wao katika uwekezaji na umiliki wa mali, ndivyo msingi wa uchumi shirikishi na endelevu unavyozidi kuimarika.