Tabora. Chama cha Madereva Bodaboda Mkoa wa Tabora umewaonya wanachama wake kutobeba abiria wanaokwenda nje ya mji nyakati za usiku wakihofia usalama wao.
Uamuzi huo unakuja baada ya kurejea tena kwa matukio ya uhalifu kwa sura nyingine ya kutegewa waya barabarani usiku, kuuawa na pikipiki zao kuchukuliwa.
Akizungumza leo Machi 24, 2026 Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Tabora, Mrisho Shime amesema baada ya Polisi kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne wa mauaji ya bodaboda, matukio hayo yalikoma lakini yameanza tena.
“Mwanzoni tulikuwa tunakatwa sana na vitu vyenye ncha kali na pikipiki inachukuliwa au kuporwa tu pikipiki na kutelekezwa porini, sasa hivi unategewa kamba unaanguka, unauawa na pikipiki inachukuliwa,” amesema.
Amedai kwa kipindi cha Januari mpaka Machi 2026 zaidi ya bodaboda watano wameuawa kwa namna mbalimbali lakini pikipiki zaidi ya 10 zimeporwa na madereva kujeruhiwa vibaya, kwa hiyo mazingira hayo yanawapa bodaboda hofu ya kufanya kazi wakati wote kama ambavyo wanatamani.
“Yaani idadi hiyo kwa watu mliozoeana, mnashinda pamoja kwenye kazi zenu halafu unaona ghafla mwenzio kauawa hapo amekatwakatwa, pikipiki zenyewe ni za mikataba zinaporwa ni changamoto sana hatujui tufanye nini ambacho ni bora kwa usalama wetu,” amesema.
Amesema mwisho wa wiki iliyopita mtumiaji wa kawaida wa bodaboda ambaye sio mwanachama wao alitegewa waya barabarani akaanguka kaumizwa vibaya na kapoteza vitu.
“Inawezekana walimtega wakijua ni bodaboda lakini kumbe alikuwa ni mtu mwingine tena mzee mtu mzima kabisa wakamuangusha vile,” amesema.
Jambo ambalo amesisitiza ni kwamba vyombo vya usalama mkoani humo viangalie pia kwa nini kipindi mishahara ikiwa imetoka uhalifu unapungua na hakuna bodaboda anayeuawa wala kuporwa, lakini tarehe za katikati ya mwezi usalama unakua mdogo kwa madereva hao.
Twaha Ramadhani ni dereva bodaboda ameiomba Serikali kutazama maisha yao juu ya usalama wao na pia ijulikane kama usafirishaji ni ajira kama ajira zingine.
“Yaani namna tunavyopigwa na kuuawa utadhani ni kundi la tofauti kabisa na Taifa hili, wakati tunachangia mapato na tuna familia zetu tunaziendesha kwa kazi hiihii,” amesema.
Kwa upande wa dereva, Saidi Ally ambaye mara kadhaa pia amekua akishiriki misako ya kupotea kwa wenzao, amesema operesheni kwa ajili ya kunusuru kundi hilo zinapaswa kuwa endelevu kwa sababu wahalifu wapo kila siku.
“Kama ambavyo wahalifu wapo kila siku kutuumiza basi inapaswa hata operesheni na misako ya wahalifu iwe kila wakati,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema bodaboda waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kama ambavyo wamekuwa wakifanya wakati wote, kwa kutoa taarifa za viashiria na vitendo vya kihalifu lengo ni kuhakikisha wanakua salama.
“Sisi tupo kazini wakati wote na tutahakikisha wahalifu wote wanaosumbua kundi hili muhimu kwenye sekta ya usafirishaji tunawatia nguvuni na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria,” amesema.
