VUNJO.
MBUNGE wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, Enock Koola ameendelea na ziara yake ya kuhamasisha kilimo cha kahawa katika jimbo hilo ambapo mamia ya wakulima wakijitokeza kushiriki na kupata elimu kuhusu mbinu bora za uzalishaji wa zao hilo la kimkakati.
Katika mwendelezo wa ziara hiyo, Mbunge pamoja na timu yake ilitembelea kata za Mwika Kaskazini na Mamba Kaskazini, akiambatana na Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Catherine Joachim pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava kuhamasisha wakulima wa zao la kahawa.
Akizungumza na wananchi, Koola alisisitiza umuhimu wa kufufua na kuimarisha kilimo cha kahawa kama nguzo kuu ya uchumi wa wananchi wa Vunjo.
Alibainisha kuwa juhudi za pamoja kati ya serikali, viongozi wa kisiasa na wakulima ni msingi wa kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa kahawa, na kuhakikisha wakulima wanapata masoko yenye tija.
Kwa upande wake, Dkt. Catherin Joachim aliwahimiza wakulima kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya kahawa kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo na kutumia mbinu za kisasa ili kuongeza tija na kipato.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mnzava, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kupitia vyama vya ushirika pamoja na matumizi sahihi ya pembejeo ili kuongeza ushindani wa kahawa ya Vunjo katika soko la ndani na kimataifa.
Wakulima wamepongeza jitihada za Mbunge kwa kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha zao la kahawa linakuza uchumi wa kaya na maendeleo ya jamii katika eneo hili.
.jpeg)
.jpeg)

