Mfanyakazi wa shambani aliyemuua mtoto wa mwajiri wake, ahukumiwa kunyongwa

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Bukoba, imemuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyekuwa mfanyakazi wa shambani, Erick Christian baada ya kukutwa na hatia ya kumuua mtoto wa mwajiri wake, aliyekuwa na umri wa miaka saba, Honorata Justinian.

Kabla ya kumuua mtoto huyo, mshtakiwa huyo aliiba luninga na nguo nyumbani kwa baba wa mtoto huyo, Justinian Baserwa, ambapo pia waligundua mtoto wao amepotea na baadaye kukuta mwili wake ukiwa shambani.

Hukumu hiyo ilitolewa Machi 19, 2026 na Jaji Lilian Itemba, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo.

Jaji Itemba amesema mahakama imeridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kosa hilo bila kuacha shaka yoyote, kufuatia tukio lililotokea Aprili 5, 2024 katika Kijiji cha Rugela, Wilaya ya Karagwe, Mkoa wa Kagera.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, mshtakiwa ambaye awali alikuwa akiishi na kufanya kazi katika familia ya marehemu, alikamatwa akiwa na televisheni iliyoibiwa kutoka nyumbani kwa baba wa marehemu Justinian.

Mahakama ilielezwa kuwa siku ya tukio, baba wa marehemu alikuwa shambani alipopokea taarifa ya kukamatwa kwa mtu aliyekuwa na televisheni yenye utata.

Aliporudi nyumbani, alibaini kuwa televisheni na baadhi ya mali zilikuwa zimeibwa, pia binti yake haonekani hapo nyumbani.
Baada ya msako, mwili wa mtoto huyo ulipatikana katika shamba jirani ukiwa na dalili za kushambuliwa kingono na baadaye kuuawa kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi wa daktari.

Katika kuthibitisha kesi hiyo upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 10 na vielelezo sita.

Shahidi wa nne, Justinian (baba wa marehemu) alisema akiwa shambani kwake akivuna mahindi alipokea simu kutoka kwa shahidi wa tano, Kalisti Kayumbu ambaye ni mgambo, akimjulisha kwamba wamemkamata mwizi aliyekuwa na luninga.

Shahidi huyo aliwaomba wamzuie mshukiwa huyo huku akirudi nyumbani ili kuona kama luninga hiyo ilikuwa yake, nyumbani kwake, aligundua kuwa televisheni yake na nguo zake hazipo.

Alidai alipokuwa njiani kwenda Polisi, mkewe alipiga simu na kumwambia binti yao, Honorata amepoteza kwani haonekani hapo nyumbani ambapo alilazimika kurudi haraka na kujiunga na majirani kumtafuta mtoto wao, waliupata mwili wa binti yake katika shamba karibu na mpaka wa ardhi ya jirani yake.

Shahidi huyo alienda kuripoti wizi wa luninga na mauaji ya binti yake, ambapo baada ya mshtakiwa kukamatwa alisema alikuwa akiishi na kufanya kazi katika shamba lake kwa miezi mitatu na mara nyingi alikuwa akienda kutazama luninga nyumbani kwake.

Shahidi wa kwanza, aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu alieleza kubaini kuwa mwili huo ulitoka damu kutoka puani na uke na dalili za jeraha kwenye eneo la sehemu za siri na kuwa ilionyesha uwezekano wa kushambuliwa kingono, na kuhitimisha kuwa chanzo cha kifo hicho kilikuwa kukosa hewa.

Shahidi wa pili, Sajenti Emmanuel alisema mwili wa marehemu ulipatikana takriban mita arobaini na mbili kutoka nyumbani kwa familia yake.

Shahidi wa tano, Kalist alisema siku ya tukio alimaliza kuoga mtoni ghafla, alikutana na mshtakiwa akitoka kwenye vichaka huku akiwa amebeba luninga na alipomuuliza kuhusu alikoipata,   alitoa maelezo ambayo yalizua shaka na pia aliona madoa ya damu usoni mwa mshtakiwa.

Uamuzi Jaji

Akitoa hukumu, Jaji Itemba alisema ushahidi wa kimazingira uliowasilishwa na upande wa mashtaka uliunda mnyororo kamili unaoonyesha bila shaka kuwa mshtakiwa ndiye aliyefanya mauaji hayo.
Mahakama pia ilibaini kuwa mauaji hayo yalifanyika kwa nia ovu, ikizingatiwa ukatili uliotumika dhidi ya mtoto huyo, ikiwemo unyanyasaji wa kingono na kufa kwa kukosa hewa.
Kutokana na hali hiyo, mahakama ilimuhukumu mshtakiwa kunyongwa hadi kufa kwa mujibu wa sheria na kuamuru luninga iliyokamatwa irejeshwe kwa mmiliki wake halali, Justinian.

“Naona upande wa mashtaka umethibitisha kesi yake dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote kwa hiyo naona mshtakiwa Erick Christian ana hatia ya kosa la mauaji kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu. Hukumu ni moja tu iliyotolewa kwa kosa la mauaji kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu ,mshtakiwa anahukumiwa kunyongwa hadi kufa,” Jaji alihitimisha.