Dar es Salaam. Kukamilika kwa mradi mpya wa majengo ya makazi ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), uliopo Canadian Masaki jijini Dar es Salaam umegeuka kuwa wa aina yake baada ya kuwekwa mfumo wa kielektroniki kwenye milango.
Mfumo huo utatumiwa kusetiwa na maofisa wa IT wa wakala kwa mteja asiyelipa kodi hivyo hatoweza kuingia ndani hadi pale atakapolipa.
Hatua hiyo inafuatia uwepo wa baadhi ya wateja wanaosua sua kulipa kodi katika nyumba za Serikali zilizopo maeneo mbalimbali hapa nchini.
Hayo yote yamedhihirika hii leo Jumanne Machi 24, 2026 katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Masanja Kadogosa.
Katika mradi huo hadi sasa yameshakamilika majengo matatu kati ya 18 yanayojengwa kwa fedha za ndani.
Akizungumzia ziara hiyo mara baada ya ukaguzi Mwenyekiti Kadogosa amesema kila jengo linaweza kubeba familia 12 ambapo kila apatimenti moja kwa mwezi ni Sh4.5 milioni.
“Lengo la makazi kama haya ni watu kuweza kumudu. Tumewapa maagizo TBA na kuna awamu ya ujenzi mwimgine unaoanza mwaka mpya wa fadha” amesema.
Kadogosa amesema lengo ni kutaka taasisi za umma kuja na mifumo itakayowafanya waondoe utegemezi kwenye bajeti kuu ya Serikali.
“Thamani ya fedha na majengo yenyewe kama kamati timeridhishwa na tunawapongeza TBA,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Charles Msonde amesema katika mradi huo yatajengwa majengo 18 na kila jengo litaweza kubeba familia 12.
Amesema kwanzia mwaka ujao wa fedha 2026/27 yataanza kujengwa pia majengo mengine manne kwaajili ya wananchi wote wakiwemo na watumishi wa umma.
“Mradi wa uendelezaji wa Canadian Village ni mpango mkakati kwaajili ya kutosheleza wakazi takribani 406, Majengo haya matatu yamekamilika na yameshapangwa,” amesema.
Amesema mtu yeyote akitaka jengo anatoa oda anatanguliza fedha anajengewa kisha baada ya miaka miwili anakabidhiwa jengo lake.
Aidha, TBA imesema gharama za utekelezaji wa mradi jengo moja Sh4.6 bilioni ambapo majengo yote ni Sh13.7 bilioni.
