Dar es Salaam. Uwekezaji wa fedha katika kushughulikia ugonjwa wa kifua kikuu (TB) nchini Tanzania bado haujitoshelezi, hali inayochangia kuendelea kuwepo kwa maambukizi mapya na vifo vinavyoweza kuzuilika, licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali na wadau wa maendeleo.
Takwimu zinaonesha Tanzania inachangia takribani asilimia 22 pekee ya fedha zote za mapambano dhidi ya TB, huku wafadhili wakichukua sehemu kubwa ya mzigo huo.
Hayo yanajiri ikiwa Machi 24 ya kila mwaka ni Siku ya TB Duniani. Siku hiyo (ambayo ni leo, Jumanne) ilianzishwa kukumbuka tukio muhimu la mwaka 1882, ambapo mwanasayansi Robert Koch aligundua bakteria wanaosababisha TB. Ugunduzi huo ulikuwa hatua kubwa katika kupambana na ugonjwa huo.
Lengo la kuanzishwa kwa Siku ya TB lilikuwa kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo, kuhamasisha watu kupima na kupata matibabu mapema, kupunguza unyanyapaa kwa wagonjwa na kuhimiza juhudi za dunia kumaliza ugonjwa huo.
Kupitia Global Fund, nchi hupokea asilimia 60 ya fedha, wakati wadau wengine wa maendeleo, wakiwemo USAID, wakichangia asilimia 18. Hali hii inaifanya sekta ya TB kutegemea zaidi misaada ya nje, jambo linalotia shaka uendelevu wa huduma hizo endapo ufadhili utapungua.
Kwa mujibu wa wataalamu, pengo la fedha linaathiri moja kwa moja huduma za msingi, kama uchunguzi na ufuatiliaji wa wagonjwa.
Alipoulizwa kuhusu nchi imejipangaje kushughulikia changamoto ya ugharamiaji wa huduma za kifua kikuu, hasa katika wakati huu ambao wafadhili wengi wanajitoa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe, amesema: “Serikali ilishajipanga, na tangu tunazungumzia ugharamiaji wa VVU/Ukimwi tulishaanza kujipanga kushughulikia kifua kikuu.
“Serikali inalipia wananchi wake. haiwezi kuacha watu wake wapate shida, itatoa fedha kugharamia,” amesema.
Daktari anayehusika na huduma za TB kutoka Health Promotion Tanzania, Kuduishe Kisowile, anabainisha kuwa kwa sasa hata watoto wanaougua nimonia hawapimwi TB kama ilivyokuwa awali, kutokana na ukosefu wa rasilimali.
Aidha, programu za kuwatafuta wagonjwa (outreach) zimepungua kwa sababu ya ukosefu wa fedha za usafiri na motisha kwa wagonjwa, hali inayosababisha baadhi ya waathirika kubaki bila kugundulika.
Changamoto hizo zinabaika wakati ambapo ugonjwa wa TB bado ni tishio kubwa nchini. Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye mzigo mkubwa wa TB duniani, ikiwa na takribani wagonjwa 118,000 mwaka 2024 na vifo 17,000.
Kwa kila watu 100,000, watu 183 wanakadiriwa kuugua TB. Hali hii inaendana na takwimu za dunia zinazoonyesha watu milioni 10.7 waliugua TB mwaka 2024, huku zaidi ya milioni 1.23 wakifariki bila kuwa na maambukizi ya VVU.
Katika kuelekea maadhimisho hayo, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria (UP) wamekuja na ubunifu unaoweza kubadilisha mfumo wa uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu (TB), hatua inayoweza kusaidia kudhibiti kwa ufanisi zaidi janga hilo.
Kifaa hicho cha mkononi kinachoitwa MARTI kina uwezo wa kutoa uhakika wa hali ya juu kwamba mtu aliye kwenye hatari hana kifua kikuu.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Uendeshaji wa kampuni tanzu ya UP ya MARTI TB Diagnostics, Carl Baumeister, kifaa hicho ni kidogo kiasi cha kutosha kiganjani na kinahitaji tone moja la damu kufanya uchunguzi bila haja ya makohozi, sindano au maabara.
Hivi karibuni, watafiti wamekamilisha majaribio ya ndani kuthibitisha usahihi wa kipimo hicho.
Matokeo yanaonesha mafanikio makubwa katika ubainifu (specificity), unyeti (sensitivity) na usahihi wa uchunguzi.
Kifaa hicho kinakaribia kufikia viwango vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kipimo bora, hali inayokifanya MARTI kuwa chombo muhimu katika uchunguzi na utambuzi wa kifua kikuu.
‘Inaendelea kuathiri watu’
Ofisa utetezi wa masuala ya afya kutoka Health Promotion Tanzania (HDT), Julius Muhindi, anasema kifua kikuu ni ugonjwa wa muda mrefu uliodumu kwa zaidi ya miaka 100 na bado unaendelea kuathiri jamii, hasa katika mazingira yenye msongamano wa watu na uingizaji hewa duni.
Anaeleza kuwa takribani asilimia 25 ya watu duniani wana maambukizi fiche (latent TB), ambayo hujitokeza pale kinga ya mwili inaposhuka.
Anabainisha kuwa mtu mmoja mwenye TB ambaye hajaanza matibabu anaweza kuwaambukiza watu kati ya 10 hadi 15 kwa mwaka, hali inayochangia kuenea kwa ugonjwa huo kimyakimya.
Hata hivyo, bado kuna changamoto ya kugundua wagonjwa mapema, ambapo takribani asilimia 24 ya wagonjwa hawafikiwi wala kutambuliwa na mfumo wa afya.
Mbali na changamoto za kifedha, sababu nyingine zinazochangia kuendelea kuwepo kwa TB ni pamoja na maambukizi ya VVU, lishe duni, magonjwa kama kisukari, pamoja na matumizi ya pombe na uvutaji sigara. Pia, imani potofu kuwa kila mgonjwa wa TB ana VVU imeendelea kuwazuia baadhi ya watu kujitokeza kupima na kupata matibabu.
Katika maeneo ya wafugaji, unywaji wa maziwa yasiyochemshwa umetajwa kuwa chanzo kingine cha maambukizi ya TB, ambapo bakteria kutoka kwa ng’ombe huweza kuingia kwa binadamu kupitia maziwa hayo.
Pamoja na jitihada zilizopo, Tanzania imefanikiwa kupunguza maambukizi ya TB kwa asilimia 40 na vifo kwa asilimia 68 katika baadhi ya viashiria, lakini bado iko nyuma ya malengo ya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Kwa ujumla, upungufu wa maambukizi umefikia asilimia 12 pekee, dhidi ya lengo la asilimia 50, huku vifo vikishuka kwa asilimia 29, dhidi ya lengo la asilimia 75.
Wataalamu wanaeleza kuwa ili kufikia lengo la kutokomeza TB, kuna haja ya kuongeza uwekezaji wa ndani, kuimarisha bima ya afya kwa wote ili kurahisisha upatikanaji wa huduma, pamoja na kuwekeza katika viwanda vya ndani vya dawa na vifaa tiba ili kupunguza utegemezi wa nje.
Aidha, kurejesha ushiriki wa jamii, ikiwa ni pamoja na waganga wa jadi na mashirika ya kiraia yaliyokuwa mstari wa mbele katika ugunduzi wa wagonjwa, kunaweza kusaidia kuongeza kasi ya kubaini maambukizi mapema na kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.
