Real Admiral Hassan Awataka Wataalam Uokoaji Kufanya Kazi Kwa Weledi

Bakari Mahundu
March 24, 2026
0 Comments

Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Real Admiral Ameir Ramadani Hassan, amewataka wataalam wa zimamoto na uokoaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutekeleza majukumu yao kwa weledi pindi majanga mbalimbali yanapotokea nchini.

Real Admiral Hassan ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha wataalam wa zimamoto na uokoaji wa JWTZ kilichofanyika katika ukumbi wa Kikosi cha Usafirishaji Mwanza (MTC), tarehe 23 Machi 2026.

Amesisitiza kuwa mafunzo, vifaa na utayari wa kukabiliana na majanga ni jambo muhimu katika kuhakikisha wanakuwa tayari wakati wote majanga yanapotokea.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kukabiliana na Majanga, Kanali Juma Emmanuel Katunge, amesema kuwa Makao Makuu ya Jeshi yameandaa kikao hicho ili kuwajengea uwezo wataalam wake na kupata uelewa wa pamoja juu ya majukumu yao.

Wataalam wa zimamoto na uokoaji jeshini wamekuwa wakishiriki katika operesheni za uokozi wakati wa majanga ya asili na ajali mbalimbali kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali.

Kikao kazi cha wataalam wa zimamoto na uokoaji wa JWTZ kinafanyika kuanzia tarehe 23 hadi 26 Machi 2026.

Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Real Admiral Ameir Ramadani Hassan