Ripoti yabaini pengo la upatikanaji maji, licha ya uzalishaji kuongezeka

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wananchi wakihaha kupata maji safi, ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imebaini maji yaliyopo yalitosheleza asilimia 52 tu ya mahitaji katika mwaka wa fedha 2024/25.

Ripoti hiyo inaonesha uzalishaji wa maji uliongezeka kwa asilimia 19, huku mahitaji yakiongezeka kwa asilimia 4.5 ikilinganishwa na mwaka 2023/24. Uwiano wa uzalishaji dhidi ya uwezo wa mitambo umefikia asilimia 58 kutoka asilimia 53, lakini mahitaji yalifikia asilimia 89 ya uwezo huo.

Hali hiyo inaashiria kuwa hata miundombinu iliyopo ikitumika kikamilifu bado haiwezi kukidhi mahitaji, hivyo kuhitaji uwekezaji zaidi katika sekta ya maji.

Waziri wa Maji, Juma Aweso, amesema Serikali inaandaa mazingira rafiki kwa sekta binafsi kushiriki katika utoaji wa huduma za maji kupitia mabadiliko ya sera na sheria. Pia amesema teknolojia ipo ya kuyafanya maji yenye chumvi yafae kwa matumizi ya binadamu.

Changamoto hiyo inaonekana kwa wananchi, ambapo mkazi wa Tabata, Dar es Salaam, Milfat Juma amesema kwa muda mrefu hapati maji ya bomba na hulazimika kutegemea mvua.

Jijini Mbeya, wakazi wa maeneo ya Isyesye, Soweto, Ilemi, Iganzo, Ilomba na Kagera wamelalamikia uhaba wa maji, huku matumaini yakiwekwa kwenye mradi wa maji wa mto Kiwira unaogharimu zaidi ya Sh119 bilioni na umefikia asilimia 49 ya utekelezaji.

Morogoro, mkazi wa Mtaa wa Mkundi, Jamsin Yassin, amesema hupata maji mara moja au mbili kwa wiki, na wakati mwingine hulazimika kununua dumu la lita 20 kwa Sh500 au kusubiri maji usiku kucha bila mafanikio.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Mwalimu Samson Sombi, amesema changamoto si uzalishaji pekee bali ni uwiano kati ya mahitaji, miundombinu na usambazaji.

Amesema Serikali inapaswa kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya uzalishaji na uhifadhi wa maji pamoja na kuboresha mtandao wa usambazaji ili kupunguza upotevu.

Licha ya changamoto hizo, ripoti inaonesha mafanikio ikiwemo ongezeko la uwezo wa uzalishaji kutoka mita za ujazo milioni 736 hadi milioni 795, uzalishaji kuongezeka hadi mita za ujazo milioni 464, na idadi ya wateja wa maji kufikia 1,812,712.

Aidha, wateja wa huduma za majitaka wameongezeka kutoka 56,691 hadi 62,314.