Tanzania Mnufaika wa Mpango wa TEF wa Ujasiriamali Afrika 2026

Tanzania imepata uwakilishi miongoni mwa wanufaika wa Mpango wa Ujasiriamali wa Taasisi ya Tony Elumelu (TEF) wa mwaka 2026, huku wajasiriamali 12 wakichaguliwa katika kundi la kwanza la washindi waliotangazwa barani Afrika.

Hayo yalitangazwa Transcorp Hilton Abuja, ambapo wajasiriamali 1,951 walibainishwa kama sehemu ya wanufaika wapatao 3,200 watakaosaidiwa na TEF kwa mwaka huu.

Uteuzi huo wa wanufaika wa mpango huo ulifuatia mchakato uliokuwa na ushindani mkubwa, ambao ulivutia zaidi ya waombaji 260,000 kutoka nchi 54 za Afrika.

Kundi la mwaka 2026 litatangazwa kwa awamu ili kukuza ushirikishwaji na kupanua ushiriki wa kisekta. Kundi la kwanza linajumuisha wajasiriamali wapatao 1,951 waliochaguliwa chini ya Mpango wa Kina wa TEF.

Makundi mengine yatakayotangazwa baadaye mwaka huu ni pamoja na wajasiriamali 100 chini ya Mpango wa Kudhibiti Taka, wajasiriamali 100 chini ya Mpango wa Aguka nchini Rwanda, na wajasiliamali 1,049 chini ya Mpango wa Wanawake wa Afrika, ambapo ushiriki kutoka Tanzania unatarajiwa kuongezeka.

Kila mjasiriamali aliyechaguliwa atapokea kiasi cha $5,000 (sawa na kama Sh12,950,000 hivi) katika ufadhili wa mbegu, pamoja na mafunzo ya biashara, ushauri, na ufikiaji wa mtandao wa Afrika nzima, unaolenga kuharakisha ukuaji wa biashara na fursa za ajira kupitia mfumo wa kina wa usaidizi.

Kujumuishwa kwa Tanzania katika kundi hili kunaonyesha ushiriki wake unaoendelea katika mfumo wa ikolojia wa ujasiriamali Afrika, huku pia ukiangazia fursa ya uimarishaji zaidi wa ushindani katika mizunguko ya maombi hapo baadaye.

Barani Afrika, wanawake ni asilimia 51 ya wajasiriamali waliochaguliwa, ikilinganishwa na asilimia 49 ya wanaume, hii ikionyesha dhamira ya TEF ya kuzingatia usawa wa kijinsia.

Akizungumza wakati wa hafla, Tony Elumelu alieleza jukumu muhimu la ujasiriamali katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kushughulikia ukosefu wa ajira kwa vijana katika bara zima la Afrika.

Alisisitiza pia umuhimu wa kuweka mazingira ya kusaidia mafanikio ya biashara.

Mwanzilishi mwenza Awele Vivian Elumelu aliwahimiza waombaji ambao hawakuchaguliwa kutokata tamaa, bali waendelee kutuma maombi kwa baadaye.

Mpango wa Ujasiriamali wa TEF ni miongoni mwa mipango inayoongoza barani Afrika kusaidia wajasiriamali kupitia ufadhili, kukuza uwezo, na ushauri.

Maombi ya mzunguko unaofuata yamefunguliwa kwa sasa. Watanzania, pamoja na Waafrika wengine, wanahimizwa kutuma maombi yao kabla ya mwisho wa Machi 2026. Kwa habari zaidi, tembelea: www.tonyelumelufoundation.org.