Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imewahakikishia wawekezaji kuwepo kwa mazingira bora, ya haki na yanayotabirika katika mfumo wa kodi kufuatia dhamira ya kutekeleza kikamilifu mapendekezo 284 ya maboresho ya mfumo wa kodi yaliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Uhakikisho huo umetolewa wakati wa Mkutano wa Kubadilishana Uzoefu na Mafunzo ya Kodi kati ya Tanzania na kampuni za China wa mwaka 2026 uliofanyika jana, Jumatatu Machi 23, 2026, ukileta pamoja Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wawekezaji kutoka China.
Katika mkutano huo, wadau walijadili mageuzi ya mfumo wa kodi yanayolenga kuongeza uwazi, usawa na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato huku yakilenga pia kuimarisha imani ya wawekezaji, hasa kutoka China ambayo imeendelea kuwa mshirika mkuu wa uwekezaji nchini.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema mamlaka hiyo imejipanga kutekeleza mapendekezo yote 284 kwa awamu tatu ambazo ni muda mfupi, wa kati na wa muda mrefu.
“Napenda kuwahakikishia wafanyabiashara, wawekezaji na wanadiplomasia kwamba TRA itatekeleza kikamilifu mapendekezo yote 284 kama ilivyoelekezwa na Rais,” amesema.
Amesema lengo la mageuzi hayo ni kujenga mfumo wa kodi wa kisasa, wenye haki na unaotabirika ambapo walipa kodi wote wanatendewa sawa bila kujali ukubwa wa biashara au asili yao.
“Tunalenga kuhakikisha wote wanaostahili kulipa kodi wanafanya hivyo kwa mujibu wa sheria. Awe mfanyabiashara mdogo au mkubwa, wote wanapaswa kulipa kodi kulingana na kipato chao,” amesema.
Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chama cha Wafanyabiashara wa China na kampuni ya OASIS Financial Services Limited, ukiwa jukwaa la kujadili changamoto za kodi zilizokuwepo kwa muda mrefu pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya mamlaka ya kodi na wawekezaji.
Mwenda amesisitiza utekelezaji wa sheria za kodi utaendelea kuwa thabiti lakini wa haki, ukilenga zaidi wanaokiuka sheria badala ya kuwalenga wawekezaji kwa misingi ya uraia wao.
“TRA haina tatizo na wafanyabiashara wa China. Tatizo letu ni kwa kampuni chache ambazo hazizingatii sheria za kodi,” amesema.
Ameongeza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuboresha huduma kwa walipa kodi, kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kikodi na kuongeza uwazi katika usimamizi wa kodi.
Miongoni mwa mageuzi yanayopewa kipaumbele ni pamoja na kidijitali ya mifumo ya kodi, uratibu bora wa ukaguzi wa kodi, tafsiri inayofanana ya sheria za kodi na uboreshaji wa huduma kwa walipa kodi.
TRA tayari imeweka mifumo ya kielektroniki katika shughuli nyingi za forodha na kodi za ndani, huku mipango ikiendelea kupanua upatikanaji wa huduma hizo kupitia majukwaa ya simu ili kurahisisha ulipaji na uwasilishaji wa taarifa za kodi.
“Tunalenga kuwa na mfumo ambao mfanyabiashara anaweza kuutumia popote alipo. Hii ni sehemu ya kutengeneza mfumo wa kodi ulio rahisi na rafiki,” amesema Mwenda.
Mamlaka hiyo pia imekiri kuwepo kwa changamoto zilizowahi kulalamikiwa na wawekezaji, ikiwamo kufanyiwa ukaguzi wa kodi mara kwa mara, makadirio ya kodi yasiyoeleweka na baadhi ya taratibu za utekelezaji wa sheria.
Hata hivyo, imeahidi kuboresha hali hiyo kwa kuimarisha uratibu wa taasisi na kuzingatia weledi katika utekelezaji wa majukumu ya kikodi.
Uhakikisho huo unakuja wakati ambapo China inaendelea kuwa chanzo kikubwa cha uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, China imekuwa ikiongoza kwa miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa katika sekta mbalimbali zikiwamo viwanda, ujenzi, usafirishaji na mawasiliano.
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema maboresho ya sera na sheria za kodi nchini tayari yameanza kuongeza uelewa kwa kampuni za China kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria za kodi.
“Maboresho ya sera na sheria za kodi nchini Tanzania yameongeza uelewa kwa kampuni za China kuhusu ulipaji wa kodi na kuimarisha ushirikiano wao na TRA,” amesema.
Amesema Serikali ya China itaendelea kuhamasisha kampuni zake zinazofanya biashara Tanzania kuheshimu sheria za kodi na kushirikiana kikamilifu na TRA.
“Tunahimiza kampuni zote za China kulipa kodi kwa mujibu wa sheria, kuepuka ukwepaji wa kodi na kushirikiana kikamilifu na TRA,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya OASIS Financial Services Limited, Stambuli Myovela, amesema mageuzi yanayoendelea katika mfumo wa kodi tayari yameanza kuimarisha mazingira ya biashara nchini.
Amesema hatua hizo zimechangia kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza Tanzania huku changamoto zilizokuwepo zikishughulikiwa hatua kwa hatua.
“China ni mwekezaji mkubwa nchini, hivyo ushirikiano wa kikodi kati ya TRA na kampuni za China una umuhimu mkubwa kwa uchumi wetu,” amesema.
Ameongeza kuwa majadiliano kama hayo yanasaidia kutatua changamoto zilizokuwa kikwazo kwa wawekezaji na kuleta suluhisho la pamoja.
Katika kipindi cha miezi nane iliyopita, TRA imekusanya takribani Sh24.5 trilioni, mafanikio ambayo Mwenda amesema yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na utiifu wa walipa kodi, wakiwamo wafanyabiashara wa China.
“Haya yasingewezekana bila ushirikiano wa wafanyabiashara. Tunawashukuru kwa mchango wao katika kulipa kodi,” amesema.
Mmoja wa wawekezaji kutoka China aliyeshiriki mkutano huo amesema mageuzi ya mfumo wa kodi yanaashiria kukua kwa mazingira ya uwekezaji nchini.
“Mifumo ya kodi sasa inaeleweka zaidi na imeanza kuwa ya kidijitali. Hii inapunguza sintofahamu kwa wawekezaji na kutusaidia kupanga mipango ya muda mrefu,” amesema.
