Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameeleza mpango wake wa kutaka kuagiza gesi asilia kutoka Msumbiji ikiwa ni juhudi za kukabiliana na uhaba wa rasilimali hiyo nchini mwake, ambapo miundombinu yake imeharibiwa kutokana na vita dhidi ya Urusi.
Zelensky amefanya mazungumzo na mwenzake wa Msumbiji, Rais Daniel Chapo, jana Jumatatu Machi 23, 2026 na kueleza hatua yake mpya kutaka kuagiza gesi asilia kutoka katika nchi hiyo inayopakana na Tanzania upande wa kusini.
Baada ya mazungumzo hayo, Zelensky aliandika kwenye mtandao wa X kwamba Ukraine inaweza kuisaidia Msumbiji kukabiliana na changamoto za kiusalama kwa kubadilishana na usambazaji wa gesi.
Ukraine imeonyesha nia ya kuagiza gesi asilia kutoka Msumbiji, kutokana na mashambulizi ya Urusi kuathiri rasilimali zake za nishati.
“Ukraine ina nia ya kupata vyanzo vya ziada vya nishati. Msumbiji ina nia ya uzoefu na teknolojia za Ukraine ili kuimarisha usalama wa ndani na kulinda watu dhidi ya ugaidi,” Zelensky ameandika.
Msumbiji imekuwa ikikabiliana na uasi wa wanamgambo wenye itikadi kali za kijihadi tangu mwaka 2017.
Kwa mujibu wa Reuters, kabla ya uvamizi wa Urusi mwaka 2022, uzalishaji wa ndani wa gesi wa Ukraine ulikidhi karibu mahitaji yake yote. Hata hivyo, katika miaka minne iliyopita, mashambulizi ya Urusi yameharibu miundombinu ya uzalishaji.
Mwishoni mwa mwaka jana, Gavana wa Benki Kuu, Andriy Pyshnyi, alisema kuwa Ukraine imepoteza takriban nusu ya uzalishaji wake wa gesi.
Msumbiji ni mzalishaji mkubwa wa gesi barani Afrika, na miradi inayoendelea na kampuni za TotalEnergies na Eni, inaweza kuongeza mauzo ya nje ya nchi hiyo kupitia mpango huo iwapo utaanza kutekelezwa.
Kampuni kubwa ya mafuta ya Ufaransa, TotalEnergies, ilizindua tena mradi wake wa gesi wenye thamani ya Dola bilioni 20 mwezi Januari, ikiwa ni miaka mitano baada ya kusitishwa kufuatia shambulio la wanamgambo wa kijihadi.
