Tabora. Serikali imeanza rasmi kampeni ya chanjo ya ugonjwa wa polio mkoani Tabora inayolenga kuwafikia zaidi ya watoto milioni moja wenye umri chini ya miaka 10, katika jitihada za kuzuia na kutokomeza kabisa ugonjwa huo hatari unaosababisha kupooza kwa viungo.
Uzinduzi wa shughuli hiyo umefanyika leo Machi 24, 2026 katika Shule ya Msingi Majengo, Kata ya Mpela, Manispaa ya Tabora, ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Wella amesema kampeni hiyo itatekelezwa kwa awamu ya kwanza hadi Machi 27 mwaka huu, huku akitoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wenye sifa wanapatiwa chanjo hiyo.
Amesema mafanikio ya kampeni hiyo yanategemea ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo asasi za kiraia, makundi ya kijamii na vyombo vya habari katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo.
Mkuu wa wilaya ya Tabora, Upendo Wella akizungumza wakati wa uzinduzi wa chanjo ya Matone ya Polio katika shule ya msingi Majengo manispaa ya Tabora
“Kumekuwepo na baadhi ya wazazi na walezi wenye dhana potofu kuhusu chanjo wakiamini kuwa zina madhara. Huu ni wakati wa kuendelea kutoa elimu ili watoto wetu waweze kupata chanjo na kulindwa dhidi ya ugonjwa wa polio,” amesema.
Aidha, amezitaka halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha chanjo hiyo inapatikana katika vituo vyote vya afya ili kufikia lengo la kuwachanja asilimia 100 ya watoto waliokusudiwa.
Pia amewaagiza watumishi wa sekta za afya na elimu kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa shughuli hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Ofisa Programu wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Bonaventura Nestory amesema Mkoa wa Tabora una idadi kubwa ya watoto walengwa wa chanjo hiyo, hivyo unahitaji juhudi kubwa kuhakikisha wote wanafikiwa.
Amesema umuhimu wa kampeni hiyo unaongezeka kufuatia kubainika kwa viashiria vya virusi vya polio katika sampuli za maji taka zilizochukuliwa katika Wilaya za Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza.
“Hii inaonesha bado kuna hatari ya uwepo wa virusi vya polio, hivyo ni muhimu wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vilivyotengwa kwa ajili ya chanjo,” amesema.
Mkuu wa wilaya ya Tabora, Upendo Wella akitoa chanjo kwa mmoja wa watoto waliopelekwa na wazazi wao kupata chanjo hiyo katika shule ya msingi Majengo manispaa ya Tabora
Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la Tanzania Interfaith Partnership (TIP), Salim Ibwe amesema wadau wa chanjo wameweka jumla ya wahamasishaji 2,500 mkoani humo ili kusaidia kuwafikia walengwa.
“Tumesambaza wahamasishaji hawa katika maeneo mbalimbali ya mkoa ili kuhakikisha wazazi wanapata taarifa na kuwapeleka watoto wao kupata chanjo,” amesema.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Honoratha Rutatinisibwa amesema wamepokea zaidi ya dozi milioni 1.5 za chanjo ya polio kutoka Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo.
Amesema pamoja na chanjo hizo, vifaa vingine vinavyohitajika katika utoaji wa huduma hiyo vimesambazwa tayari katika vituo vya afya ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi.
“Tunachohitaji sasa ni ushirikiano wa wadau wote ili kufanikisha zoezi hili na kuhakikisha watoto wote wanaostahili wanapata chanjo,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa Tabora wameeleza kuunga mkono kampeni hiyo wakisema italinda afya ya watoto dhidi ya ugonjwa wa Polio.
Mkazi wa Tabora, Mary John amesema ameupokea kwa furaha mpango huo kwa kuwa ugonjwa wa polio husababisha mateso makubwa kwa familia.