Bunge la 13 bila wakongwe

Dar es Salaam. Bunge la 13, limeendelea kupoteza wabunge wakongwe zaidi, baada ya kifo cha Mbunge wa Isimani (CCM), William Lukuvi, ikiwa ni miezi minne tangu pigo kama hilo, lilipoukuta muhimili huo muhimu kwa utunzi na usimamizi wa sheria.

Lukuvi ambaye hadi anafariki dunia alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, amehudumu nafasi ya ubunge kwa miaka 31, tangu mwaka 1995. Ndiye aliyekuwa mbunge wa muda mrefu zaidi bungeni.

Mwanasiasa huyo aliyewahi kuhudumu katika wizara mbalimbali na Ofisi ya Rais kama mshauri wa Rais wa masuala ya siasa, anakuwa mbunge wa tatu kupoteza maisha katika Bunge la 13, tangu lilipoanza Novemba 2025, linaloongozwa na Spika Mussa Zungu.

Mbunge wa kwanza kuiaga dunia katika Bunge hilo ni Jenista Mhagama, Desemba 11, mwaka jana. Hadi anafariki dunia, alishakuwa mbunge kwa miaka 25, akianza na viti maalumu mwaka 2000 na baadaye jimboni Peramiho.

Aliyekuwa mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama enzi za uhai wake.

Jenista na Lukuvi, ndio waliokuwa wabunge wa muda mrefu zaidi katika Bunge hilo, lenye jumla ya wabunge 393, wakiwemo wa majimbo na wale wa viti maalumu.

Mbali na wawili hao, mbunge mwingine wa tatu aliyefariki dunia katika Bunge hilo la 13 ni Halima Idd Nassor, aliyekuwa mbunge wa viti maalumu. Kifo chake kilitokea Januari 18, mwaka huu.

Vifo hivyo, vinalifanya Bunge la 13, liwe limepoteza wabunge watatu kwa kipindi cha miezi mitano tangu lilipoanza Novemba mwaka jana, ukilinganisha na wabunge wawili waliofariki katika Bunge la 12 ndani ya muda huo.

Katika Bunge la 12 lililoanza Novemba 13, mwaka 2020 baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo, mbunge wake wa kwanza kufariki alikuwa Martha Umbulla, Januari 21, 2021. Kipindi hicho, Bunge lilikuwa na miezi mitatu tangu kuzinduliwa.

Aliyefuatia ni Atashasta Nditiye, aliyekuwa Mbunge wa Muhambwe. Kifo chake kilitokea Februari 12, mwaka 2021. Kipindi hicho, Bunge hilo lilishakuwa na miezi mitatu tangu lizinduliwe.

Baada ya hapo, hakikutokea kifo kingine hadi miezi mitano ya Bunge hilo ilipopita. Baadaye Mei 20, 2021, akafariki mbunge wa Konde, Khatib Said Haji, aliyetokana na Chama cha ACT Wazalendo.

Hadi linamaliza muda wake wa miaka mitano, Bunge la 12 lilipoteza jumla ya wabunge 10, sawa na asilimia 2.54 ya wabunge wote 393 waliokuwepo katika Bunge hilo.

Taarifa ya kifo cha Lukuvi, imetolewa leo, Jumatano Machi 25, 2026 kupitia taarifa kwa umma, iliyotiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kifo cha Lukuvi kimetokea katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, alikokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa mshtuko wa moyo.

“Mheshimiwa Rais, anatoa pole kwa Spika wa Bunge, Mussa Zungu, familia, wananchi wa Isimani, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania kwa msiba huo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Lukuvi alizaliwa Agosti 15, 1955 katika Kijiji cha Mapogoro, Wilaya ya Iringa vijijini, mkoani Iringa. Hadi anafariki alikuwa na umri wa miaka 70.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, William Lukuvi. Enzi za uhai wake

Kifo hicho kimetangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka juu ya msiba huo wa Lukuvi aliyezaliwa Agosti 15, 1955.

Katika historia yake ya elimu, Lukuvi amewahi kusoma Tabora Teachers College (TTC) na baadaye kuhitimu Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Safari yake ya kisiasa, aliianzia ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), alipochaguliwa kuwa Mbunge wa Ismani mwaka 1995 nafasi ambayo ameendelea kushikilia hadi anafariki dunia.

Aidha, amehudumu kama waziri katika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuanzia Januari 2015 hadi Januari 2022.

Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, na Uratibu, kuanzia Novemba 2010 hadi Januari 2015. Juni 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alimteua kuwa mshauri wake wa mahusiano ya kisiasa na kijamii.

Akiwa Waziri wa Ardhi, Lukuvi alisifika kwa juhudi zake za kutatua migogoro ya ardhi nchini.

Alisimamia utoaji wa hati miliki za ardhi zaidi ya milioni mbili kwa Watanzania. Pia, katika kipindi chake ndipo alianzisha mifumo wa kutatua migogoro ya ardhi kwa kupeleka huduma karibu na wananchi.