Dar es Salaam. Jina la Doreen Mangesho linaendelea kujijenga taratibu katika tasnia ya fedha na uongozi wa taasisi, likiwa mfano hai wa namna mwanamke anavyoweza kushinda changamoto, kuleta mabadiliko chanya na kuhamasisha wengine kujiamini na kuwekeza katika ujuzi.
Kwa mtazamo wa kwanza, unaweza kuona mafanikio ya Doreen kama hadithi ya kawaida ya kupanda ngazi za taaluma.
Lakini ukisogea karibu zaidi, unagundua kuwa ni simulizi ya uthabiti, maono na mapambano dhidi ya vikwazo vinavyowakabili wanawake katika uongozi.
Doreen si tu kiongozi katika taasisi, bali pia ni mama na mlezi anayesimamia kwa umakini majukumu ya familia yake. Ndani ya majukumu haya mawili makubwa, amejenga mizani inayodhihirisha kuwa mwanamke anaweza kufanikiwa katika nyanja zote bila kuacha wajibu wake wa msingi.
Safari ya mafanikio ya Doreen ilianza baada ya kuhitimu Shahada ya Fedha na Usimamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Akiwa na ndoto kubwa ya kujenga taaluma yenye athari chanya kwa jamii, alianza kazi katika kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya KPMG kama mkaguzi wa nje.
Akiwa huko, alipata nafasi ya kufanya kazi na taasisi mbalimbali, zikiwamo benki, kampuni binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Uzoefu huo ulimfungua macho kuona namna taasisi zinavyoendeshwa, pamoja na upungufu uliokuwapo katika mifumo ya kifedha na udhibiti.
“Kupitia kazi hiyo nilijifunza mengi kuhusu mifumo ya taasisi. Lakini zaidi, niliona changamoto zilizokuwapo, jambo lililonifanya nitamani kuwa sehemu ya suluhisho, siyo tu mtazamaji wa matatizo,” anasema Doreen na kuongeza kuwa hapo ndipo wazo la kuingia kwenye uongozi lilipoanza kumjia.
Anasema alitamani kuwa katika nafasi ya kufanya maamuzi na kuleta mabadiliko halisi katika usimamizi wa fedha na uendeshaji wa taasisi.
Kutokana na maono hayo, Doreen anasema aliendelea kujijenga kitaaluma na kiutendaji hatua kwa hatua, huku akifanikiwa kuzipanda ngazi za uongozi.
Kwa sasa, ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala katika taasisi ya Private Agricultural Sector Support Trust (PASS Trust).
Katika nafasi hiyo, Doreen anasimamia idara za Fedha, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Utawala na Rasilimali Watu.
Majukumu yake yanahusisha kuhakikisha taasisi ina mkakati thabiti wa kifedha, mifumo madhubuti ya uendeshaji na rasilimali watu yenye uwezo wa kusukuma mbele malengo ya taasisi.
Aidha, anasimamia miradi inayolenga kutoa dhamana za mikopo kwa wafanyabiashara wa sekta ya kilimo, hatua inayochangia kukuza uchumi wa wananchi na kuimarisha sekta hiyo muhimu nchini.
Kwa Doreen, mafanikio hayo si tu nafasi au cheo, bali ni fursa ya kuleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya watu.
“Thamani ya kazi yangu ipo katika kuona fedha zinavyosimamiwa kwa ufanisi, miradi inavyofanikiwa na jamii inanufaika,” anasema.
Uongozi unaogusa maisha ya watu
Doreen anasema anaamini kuwa usimamizi wa fedha hauishii kwenye takwimu na hesabu, bali unapaswa kuakisi mabadiliko chanya kwa jamii. Huu ndio msingi wa falsafa yake ya uongozi—kuunganisha taaluma na matokeo halisi kwa watu.
Kupitia mtazamo huo, amejenga mifumo imara inayosaidia taasisi kufanya kazi kwa ufanisi, huku ikiendelea kuwajengea uwezo wataalamu wake.
Hata hivyo, anasisitiza matumizi ya teknolojia, uwajibikaji na uwekezaji katika rasilimali watu kama nguzo kuu za mafanikio ya taasisi yoyote.
Changamoto na namna alivyozikabili
Palipo na mafanikio hapakosekani changamoto. Safari ya Doreen nayo haikukosa changamoto. Anasema katika baadhi ya hatua za kazi yake alikumbana na upinzani uliotokana na mitazamo ya kijinsia, hususan kutoka kwa baadhi ya wanaume waliokuwa hawako tayari kuripoti kwa mwanamke.
“Nilipoteuliwa kuwa kiongozi wa idara, kulikuwa na wanaume waliotamka wazi kuwa hawako tayari kuripoti kwa mwanamke,” anakumbuka.
Badala ya kukata tamaa, anasema alichagua kujibu kwa vitendo. Alijikita katika kufanya kazi kwa weledi, kuonesha matokeo na kusimamia majukumu yake kwa uwazi na uthabiti.
Kadri muda ulivyopita, Doreen anasema upinzani huo ulianza kupungua. Waliokuwa hawaridhiki walijiondoa, huku waliobaki wakijenga timu yenye mshikamano na ufanisi.
Kutokana na uzoefu huo, Doreen anasema alijifunza kuwa uongozi si kelele, bali ni matokeo, uthabiti na uwezo wa kujenga heshima kupitia kazi.
Mizani kati ya kazi na familia
Licha ya majukumu mazito kazini, Doreen anasisitiza umuhimu wa familia katika maisha ya mwanamke.
Anasema anajiona si tu kama kiongozi wa taasisi, bali pia kama mama anayehakikisha familia yake inasimama imara.
Mwanamke huyo anaamini kuwa uongozi wa mwanamke unaanzia nyumbani katika namna anavyosimamia familia yake, kulea watoto na kuweka misingi imara ya maadili.
“Mwanamke akisimama imara, familia yake inasimama. Uongozi si katika taasisi pekee, bali pia katika familia,” anasema.
Kwa mtazamo wake, anasema kupigania ndoto na mafanikio ya kitaaluma hakupaswi kuwa sababu ya kupuuzia majukumu ya nyumbani. Badala yake, mambo hayo mawili yanakwenda sambamba kwa mipango na nidhamu ambayo mwanamke atajipangia.
Akizungumzia mafanikio yake, Doreen anataja mambo kadhaa yaliyomsaidia kufika alipo. Miongoni mwa hayo ni kuwekeza katika elimu, kujifunza kila wakati, kujituma kazini na kudumisha uadilifu.
Pia anasisitiza umuhimu wa kusoma na kuelewa nyaraka za kazi, kushirikiana na timu na kujenga uhusiano mzuri na watu wengine kazini.
Anatoa wito wa wanawake kujiamini na kuthubutu kuchangamkia fursa.
“Wanawake wengi hujihofia kuomba nafasi za juu. Ninawahimiza wajiamini na kuthubutu. Wekezeni katika elimu na jengeni mitandao ya kitaaluma,” anasema.
Anaongeza kuwa mafanikio ya mwanamke yanahitaji zaidi ya ujuzi wa kitaaluma. Yanahitaji pia uwezo wa kuwasiliana, kushirikiana na wengine na kuwa na uelewa wa kihisia.
Akimzungumzia Doreen, mtaalamu wa masuala ya uongozi, Happy Komba, anasema anasimama kama kielelezo cha mwanamke anayevuka mipaka ya vikwazo na kujenga historia ya uongozi wenye matokeo.
Anasema safari yake ni ushahidi kuwa kwa maono, bidii na uthabiti, inawezekana kubadili changamoto kuwa fursa.
“Kupitia kazi yake, si tu anajenga taasisi imara, bali pia anachangia kuinua wanawake wengine kuamini katika uwezo wao na kufikia ndoto zao,” anasema Komba.
Anasema simulizi yake inaonesha ni mwanamke anayeonesha kuwa mafanikio hayaji kwa bahati, bali kwa uamuzi wa kusonga mbele, licha ya vikwazo na kuacha alama chanya kwa watu anaowaongoza, wanaosimamiwa naye, pamoja na wale wanaomtazama.
