Leo, nabanja na Fyatu mwenzangu Donnie Tarampu usawa huu anapokongoliwa na waajemi. Nimeomba tukutane nimshaiwishi aje kwenye bara letu kuwasomba maimla wote wanaowafyatua mafyatu wao.
Japo, yeye anahangaishwa na wese, sisi pia tunalo wese ambalo ni ukwasi waliofyatua na kuficha nje. Awafyatue na kuwajengea gereza maalumu au kuwasweka Guantanamo ili watoi wetu wajao waende kuona makumbusho ya uimla.
Japo Tarampu naye ni imla kifyatufyatu, nataka nimtumie kama wale jamaa wa kule kulikoungua shoka ukabaki mpini walivyofanikiwa kumfyatua na kumtumia kuwafyatua waajemi ili wafyatue wese lao.
Nami napanga kumfunga kamba kuwa bara letu limejaza wese chini yake. Hivyo, aje achukue mizigo yetu. Licha ya wese, lina madini ya Urania na pia mamaduro kibao wanaopaswa kumadurwa haraka kabla hawajageuka kuwa bomu la nyuklia kama siyo la taka aka bomu chafu.
You know what I mean. Kama ataweza kuwamaduro walengwa, nitamshauri kaya yake ibadilishwe jina na kuitwa Tarampuland. Pia, napanga kumuuzia Fyatuland lau ajifurahishe baada ya kuzikosa Greenland na Ukanada.
Kwa vile anajua hizi shitholes zina raslimali lukuki hasa madini, najua hatakataa. Nitamuahidi kuwa nitampigia kampeni apewe tuzo ya vita, vikwazo vya kiuchumi, na ushuru wa kijembuzi na kizwazwa.
Ili kunmasa vilivyo na kumuingiza mkengge, nitamwambia kuwa mafyatu wameniibia siri kuwa akija na kuchukua mizigo yetu ili iwe yake kama Venzuela, mambo ya wizi, utekaji, upotezaji, hata unyotoaji roho vitatoweka.
Yeye kama kijogoo cha dunia, anapaswa kuwa pekee anayeweza kufanya mambo hayo. Akikubali, Mafyatu watashangilia na kumwimbia nyimbo za sifa na mapambio huku wakimramba maninihino kama chawa na kunguni wafanyavyo kwa wawafugao. Watamwita faza tena zaidi ya wanavyoimba mazee.
Nitampaka mafuta kwa mgongo wa chupa tena iliyopasuka kuwa yeye ni chaguo la Mungu na baada ya Yesu na Mtume, hakuna kiumbe bora kuliko yeye.
Nikifika kule Washingtown, nitampamba Tarampu kuwa Sir God hajawahi kuumba kiumbe smart na mwenye akili kubwa kuliko yeye. Nitamshukuru kwa kuwapasha kopakopa na ombaomba wote wanaotembeza vibakuli wakati uchumi wanao lakini wanaukalia.
Kwa vile aliwahi kufyatuliwa kura, kama alivyowahi kudai hadi akaamuru wakuda wake waiteke Kapito Hili na kukinukisha, nitamwambia kabisa.
Mizigo mingi ninayotaka aimaduro ilifyatua kura na ‘kushinda’ bila kushinda bali kushindishwa tena mingine kwa ku-shed blood. Kufanya hivyo, mingi ilifyatua mafyatu waliopinga ufyatuaji. Iliteka, ikapoteza na kudedisha wapigania uhuru.
Kuna inshu mafyatu wamenituma nimfikishie Tarampu. Kwanza, wanamhusudu hasa kiduku chake na namna anavyoweza kumuingiza mtu cha kike na asijue kama anavyofanya kwa sasa ambapo waajemi wanampeleka puta lakini anakanusha na kuwafyatua mafyatu wa Amerikia wapendao vurugu, bwimbwi, na kunyotoana roho kwa vya moto hata kwa kitu kidogo.
Pili, kwa vile anapenda vimwana, japo anasingiziwa kuwa mbaguzi, hata kama kweli, tutampa kimwana kimoja au viwili ajienjoi na kufanya kweli kutuondolea mizigo na uchuro kwa kuimaduro. Ila sitamruhusu amkaribie bi Mkubwa wangu.
Maana, anaweza kutaka kumzoea na kumsifia akaishia akamnasa vibao na kuniharibia dili hili kali. Nitamchunga kama nimchunganvyo mgoshi Machungi, yule kijogoo mwenzake wa Usoto. Kkkk!
Tatu, kwa vile ni mbabe na mwamba, nitamwambia kuwa asiruhusu kidume wala kijike chochote kujimwambafy. Kwani, dunia inapaswa kuwa na mwamba mmoja, yaani yeye na siyo vijimwamba vidogo na vichafu kama ninavyoona vimetapakaa pote. Hii inamharibia na kumvunjia heshima kama polisi na kijogoo cha dunia.
Nikifika na kupokelewa kwa kamera na vimulimuli kama kijogoo fyatu wa kweli na si wale wapokelewa mlango wa nyuma kama taka.
Lazima tukae pale Oval room tupate picha nyingi, tubanje, na tujibu maswali ya waandishi wa umbea. Kukamata vilivyo na kumuingiza mkenge aonekane ni mwenye huruma japo ni katili kama Ida sorry Idi Amin, nitagaragara chini na kulia kama wale jamaa wa Mfaranyaki nikidai kuwa kama atagoma kufyatuka na kufyatua, ajue. Mafyatu watateketea akiona. Nami nitajinyonga apoteze fyatu wa maana kama mimi.
Nne, isitoshe, kuna inshu nimenyaka. Wanapanga kwenda kwa wale jamaa wafupi wenye macho madogo ima wawauzie kaya zao au wawasaidie kuwa na bomu la nyuklia.
Kwa kuhofia kuwa jamaa wanaweza kuogopa kutoa jini kwenye chupa, wamesema wakigoma, wanakwenda kwa kiduku wa kule Koryo Kaskazini ambaye jina lake la ukoo ni Kimani ili Zungu.
Huyu mkikuyu wa Koryo acha mchezo. Hana mchezo dogo huyu mnuni. Si anamjua asivyo na dhihaka wala mchezo. Hapa, nitambana hadi aachie.
Mwisho, nitahakikisha hawa wakuda wetu wanatemeshwa bungo iwe isiwe watake wasitake. Bila hivyo, nitamwambia kuwa wasiojulikana wanaweza siku moja kumteka na kumpoteza akishastaafu.
Du! Mbona nina pingu kitandani!
