NA MWANDISHI WETU, CHWAKA
Katika kuboresha sekta ya elimu Mwakilishi wa Jimbo la Chwaka Mhe. Issa Gavu leo Machi 25,2026 amekabidhi vitabu kwa ajili ya kujisomea pamoja na vifaa mbali mbali vya elimu, lengo ikiwa ni kuleta mabadiliko katika kukuza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa skuli zote la Jimbo hilo.
Akikabidhi msaada huo Mwakilishi wa Jimbo la Chwaka, Mhe Gavu amebainisha kwamba wameamua kutoa msaada wa vifaaa mbali mbali kwa wanafunzi hao ikiwemo kompyuta mpakato,Printer, vitabu mbali mbali pamoja na mashine ya kuburuzia karatasi (Photocopy mashine) vyote vikiwa vimegharimu kiasi cha shilingi milioni 12,msaada ambao umetolewa kutoka kwa marafiki wema kwa watu wa Jimbo la Chwaka.
“Leo tumejumuika hapa kwa ajili ya kukabidhi vifaa mbali mbali kwa wanafunzi ambao wanasoma katika Jimbo la Chwaka na katika siku ya leo tumekabidhi vifaa mbali mbali ikiwemo vitabu kwa ajili ya kujisomea wanafunzi, Photocopy mashine, pamoja Printer ambavyo vitaweza kuwa ni mkombozi mkubwa kwa wanafunzi kuweza kuongeza kasi ya ufaulu katika masomo yao,”amebainisha Mhe. Gavu.
Aidha katika tukio hilo pia Mhe. Gavu kwa kushirkiana na marafiki zake wa Jimbo hilo pia wametoa msaada wa kugawa mabati katika Skuli ya Mrembo Uroa,Mashine ya kufulia nguo (Washing Machine), tanki la maji na mipira Jendele, pamoja na mafeni na vifaa vya umeme kwa Kituo cha Afya Cheju.
Gavu amesema kwamba wameamua kutoa misaada hiyo katika nyanja mbali mbali ikiwa ni moja ya hatua ya kuimarisha suala la elimu kwa wanafunzi pamoja na kuboresha afya kwa jamii ambayo inawazunguka hasa katika Jimbo la Chwaka na kuwasihi wanafunzi wasome kwa bidii,lengo ikiwa ni kuongeza maarifa ambayo yatawasaidia katika siku za usoni.

