Jeshi la Magereza nchini Tanzania limetoa kanusho kali dhidi ya taarifa zilizoandikwa na baadhi ya magazeti zikidai kuwa hali ya afya ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ni mbaya na inatia shaka.
Akizungumza kwa niaba ya Jeshi hilo, Msemaji wa Jeshi la Magereza, SACP Elizabeth G. Mbezi, amesema taarifa hizo si za kweli na zimekusudia kuleta taharuki isiyo na msingi miongoni mwa wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Jumatano Machi 25, 2026 jijini Dodoma, Jeshi la Magereza limesisitiza kuwa Tundu Lissu yuko salama na afya yake ni njema, na kwamba hakuna hali yoyote ya dharura kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

“Kimsingi taarifa hiyo siyo sahihi ni ya kuupuzwa kwani ina lengo la kuleta taharuki katika jamii. Jeshi linapenda kuujulisha umma kuwa ndugu Tundu Lissu yuko salama na afya yake ni njema,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ya Jeshi la Magereza.
Aidha, SACP Mbezi ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuzingatia maadili ya taaluma yao kwa kuhakikisha wanathibitisha taarifa kutoka kwenye vyanzo sahihi kabla ya kuzisambaza kwa umma. Amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, huku ikithamini utu na haki za binadamu kwa wafungwa na mahabusu wote.
Taarifa hiyo inakuja siku chache baada ya Tundu Lissu kuieleza Mahakama ya Rufani kuwa afya yake inaweza kuathirika zaidi kutokana na kushindwa kuhudhuria kliniki za matibabu yake akiwa mahabusu.
Katika maelezo yake, Lissu aliomba Mahakama hiyo kulisikiliza kwa dharura shauri la mapitio lililofunguliwa na Jamhuri kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliowazuia kuwasilisha ushahidi mpya katika kesi ya uhaini inayomkabili. Alieleza kuwa kuchelewa kwa shauri hilo kunasababisha kusimama kwa usikilizwaji wa kesi hiyo kwa muda usiojulikana.
Lissu aliongeza kuwa endapo shauri hilo halitasikilizwa kwa haraka, hali yake ya afya inaweza kuendelea kudorora kutokana na kukosa huduma za kiafya zinazohitajika, jambo ambalo linaweza kuathiri haki yake ya kupata matibabu na kusababisha madhara yasiyoweza kurekebishika.
Kwa sasa, Jeshi la Magereza linaendelea kusisitiza kuwa hali ya Tundu Lissu iko shwari na linawahakikishia wananchi kuwa taratibu zote za kisheria na kiutawala zinafuatwa katika kumhudumia mahabusu huyo.
