Dar es Salaam. Mbunge wa Isiman, William Lukuvi amefariki dunia, huku aliyekuwa mshindani wake katika mchakato wa ndani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa ubunge wa Isimani, Festo Kiswaga, akifunguka mambo atakayoyakumbuka.
Kumbukumbu za matendo ya Lukuvi enzi za uhai wake, zimemuibua pia mwanasiasa mkongwe, Kapteni George Mkuchika na mbunge wa zamani wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema wakimzungumzia jinsi walivyomfahamu.
Lukuvi alifariki dunia leo, Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa mshtuko wa moyo.
Mwanasiasa huyo ambaye hadi anafariki dunia alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, amehudumu bungeni kwa miaka 31, akiwa mbunge wa Isimani.
Mbali na nafasi za ubunge, Lukuvi amefariki dunia akiwa na rekodi ya kuwa waziri pekee aliyehudumu kwa muda mrefu katika wizara mbalimbali, ikiwemo ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Taarifa ya kifo chake imetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kisuluka, akimnukuu Rais Samia Suluhu Hassan, aliyesema amesikitishwa na anatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki.
“Tumepoteza kiongozi shupavu, mahiri, mwenye uzoefu mkubwa, mzalendo na mtumishi wa umma aliyelitumikia Taifa letu kwa uadilifu, weledi na kujitolea. Mchango wake mkubwa katika ujenzi na maendeleo ya Taifa letu utaendelea kuenziwa na kukumbukwa siku zote,” amesema Rais Samia.
Akizungumzia msiba huo, aliyekuwa mshindani wake katika mchakato wa ndani wa kuwania ubunge wa Isimani kupitia CCM, Kiswaga, amesema ingawa Lukuvi alikuwa mshindani wake katika mchakato huo, baada ya kuanguka aliungana naye kuhakikisha anashinda uchaguzi na kweli akashinda, kama ilivyo siku zote.
Kiswaga, amesema anamkumbuka kiongozi huyo kwa utendaji wake Isimani, kwani aliingia likiwa jipya na halikuwa na hata shule moja ya sekondari, lakini sasa zimefika zaidi ya 10.
“Amefariki dunia jimbo la Isimani likiwa na shule nyingi za msingi, zahanati, barabara, hospitali ya wilaya. Kwa sasa huwezi kutaja maendeleo ya Isimani ukaacha kutaja jina la Lukuvi,” amesema Kiswaga.
Amesema Lukuvi ni kiongozi wa kitaifa kwa sababu tangu amechaguliwa kuwa mbunge, ni kipindi kimoja pekee ndicho alihudumu nje ya baraza la mawaziri.
“Sio tu ameisaidia Isimani, pia ameisaidia nchi kwa sababu ni kiongozi aliyetokana na UVCCM. Alikuwa mtu wa watu na kama msemaji wa mkoa wa Iringa,” amesema.
Kutokana na utendaji wake, amesema isingekuwa rahisi lipangwe jambo la maendeleo linalouhusu mkoa wa Iringa, bila kumhusisha Lukuvi.
Atakavyokumbukwa na Mkuchika
Mwanasiasa Mkongwe, Kapteni George Mkuchika, amemtaja Lukuvi kuwa miongoni mwa wanasiasa mahiri na kada asiyetiliwa shaka wa CCM.
Amesema kwa pamoja waliingia kwenye siasa kwa njia zinazofanana, wote walianzia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), wakapanda hadi walipokwenda kugombea ubunge.
Mkuchika, amesema Lukuvi alikuwa mwalimu akaacha kazi hiyo, akawa Katibu wa UVCCM wilaya na kwa wakati huo haukuwa uamuzi rahisi, kwa kuwa unaacha mshahara unakwenda kujitolea.
“Alikuwa kada wa chama. Alikuwa naibu katibu mkuu wa UVCCM akaja kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya na baadaye kuwa mbunge na Wwziri,” amesema.
Amesema Lukuvi pia, aliwapenda wananchi wa jimboni kwake, kwani akiwa bungeni, kila ilipopatikana nafasi alikwenda Isimani kufanya kazi ya ubunge.
Kapteni Mkuchika pia, amemtafsiri Lukuvi kuwa mtaalamu wa sheria na taratibu za Bunge, kwa kuwa amehudumu nafasi za wizara inayoratibu shughuli za bunge kwa vipindi tofauti.
Lema, aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjii kupitia Chadema (2010-2020) ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuzungumzia kifo cha Lukuvi akisema: “Tunazaliwa bila kitu, na tunaondoka bila kitu, kifo hutukumbusha unyenyekevu wa maisha.
“Ukiyatafakari maisha kwa kina, utajifunza mengi, lakini zaidi ya yote utajifunza upendo, huruma, haki na utu wema ndio vitu vya msingi ktk kuishi.”
Lema ameendelea kusema: “Maana hapa duniani tunapita kwa kasi kubwa sana, haijalishi tunamiliki nini au sisi ni nani. Kifo ni kumbusho kuwa kesho yetu haipaswi kuwa chanzo cha maumivu kwa wengine hata kidogo.”
Katika andiko lake, Lema amesema anafikiri hiyo ndiyo maana halisi ya kuishi, kuacha alama ya wema na upendo si majeraha mioyoni mwa watu.
“Maumivu ya kuondokewa ni makubwa, lakini kumbukumbu nzuri ni tiba ya moyo. Mimi na Lukuvi tulipenda kutaniana kila tulipokutana mara zote na sasa hayupo tena. Hili pia ni kumbusho muhimu kwetu tunaondelea kuishi. Kifo hutufundisha thamani ya muda tuliobakiwa nao,” amesema Lema.
