Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imetoa ushauri na maelekezo yenye lengo la kuimarisha usimamizi wa fedha na ukamilishaji wa miradi hiyo jijini Mwanza.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) wakikagua moja ya miradi ya maendeleo ya Jiji la Mwanza
LAAC chini ya uenyekiti wa Ado Shaibu imebainisha hayo jana Jumanne, Machi 24, 2026 baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea miradi mbalimbali. Ado amebainisha maeneo kadhaa yanayohitaji marekebisho ili kuendana na matakwa ya kisheria na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Bunge imeeleza, mradi wa ujenzi wa majengo ya Idara ya Afya, Kamati imemuelekeza ofisa masuhuli kuhakikisha kiasi cha Sh527.04 milioni kilichotolewa kama malipo ya awali kwa mkandarasi kinarejeshwa.
Naibu Waziri wa Tamisemi anayeshughulikia (Elimu), Reuben Kagilwa akizungumza katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Aidha, kamati imetaka kuwepo kwa uthibitisho wa mapokezi ya fedha hizo kwa CAG kila robo mwaka kwa ajili ya uhakiki.
Vilevile, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imeombwa kupitia upya taratibu zilizotumika katika malipo ya Sh1.12 bilioni na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria kwa watumishi waliohusika na ukiukwaji wa kanuni za manunuzi.
Katika mradi wa Soko Kuu la Mwanza, Kamati imesisitiza umuhimu wa kukamilisha miundombinu ya msingi kama mifumo ya maji nje ya soko na ufungaji wa kamera za usalama (CCTV). Maelekezo hayo yanalenga kuimarisha ufanisi na usalama wa soko hilo kwa manufaa ya wafanyabiashara.
Pia, uongozi wa Jiji umepewa hadi Mei 30, 2026 kurekebisha upungufu wote ulioonekana kwenye mradi wa jengo la makazi ya mkurugenzi ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Ado Shaibu akizungumza katika moja ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza
Naibu Waziri wa Tamisemi anayeshughulikia (Elimu), Reuben Kagilwa, amepokea maelekezo hayo na kusema wizara itahakikisha yanafanyiwa kazi kwa wakati.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine, ameishukuru kamati kwa ushauri wake wa kitaalamu na kuahidi kuwa Jiji litashirikiana kikamilifu kufikia malengo yaliyokusudiwa.

