Linah alivyoagwa Kigamboni, urithi alioacha…

Dar es Salaam. Wakati familia, ndugu na waombolezaji wakimkumbuka Linah Kimaro kama mtu mcheshi na mwenye upendo wakati wa uhai wake, Jeshi la Polisi limesema linaendelea kuchunguza kwa kina chanzo cha kifo chake kilichozua maswali mengi.

Linah anayedaiwa kuuawa Machi 20, 2026 majira ya saa saba mchana kwa kuchomwa kisu na mdogo wake, Meshack, ameagwa na kuzikwa leo Jumanne, Machi 25, 2026 katika makaburi ya Kisota, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Katika ibada ya kuaga mwili wake iliyofanyika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kisiwani, waombolezaji wameelezea namna alivyokuwa mtu wa furaha, mwenye hekima na aliyependa kuwafanya wengine watabasamu.

Akisoma wasifu wa marehemu, msemaji wa familia, Herman Elinewinga amesema Linah alizaliwa Aprili 12, 1990 katika Kijiji cha Mashua, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro na alijulikana kwa upendo, hekima na tabasamu lisilokoma.

Mbali na familia, wafanyabiashara na ‘mawinga’ wa soko la Kariakoo wanasema wamkumbuka kama mshirika wao wa muda mrefu, wakieleza alivyokua kutoka kuwa ‘winga’ hadi mfanyabiashara aliyefanikiwa, huku akibaki kuwa mtu mkarimu na mchangamfu.

Kwa mujibu wa familia, safari ya kibiashara ya Linah ilianza nchini Msumbiji baada ya kuhitimu elimu ya sekondari huko, akijihusisha na biashara ya kusafirisha vyombo vya ndani kutoka Tanzania. Baadaye, alibadili mwelekeo wa biashara na kuanza kuuza nguo na viatu jijini Dar es Salaam baada ya kuolewa na Chris Kabamba.

Linah alifunga ndoa na Kabamba Februari 17, 2026 katika Usharika wa KKKT Ubungo na ameacha watoto wanne. Katika maisha yake ya biashara, alifanikiwa kujinyakulia tuzo mbili, ikiwamo Kariakoo Business Award na East Africa Business Award.

Akihubiri wakati wa ibada ya kuaga mwili huo, Mchungaji wa KKKT Kisiwani, Prosper Chao amesema kifo cha Linah kimeacha pengo kubwa kwa familia na jamii iliyokuwa ikimtegemea.

“Jamii ilimtegemea kuendelea kuishi, lakini maisha yake yamekatika ghafla kwa mazingira ambayo kila mmoja anasimulia kwa namna yake,” amesema Mchungaji Chao huku akiwataka waumini kujiandaa kiroho.

Hata hivyo Mwananchi iliotak kuzungumza na familia baada ya maziko juu ya msiba huo akiwamo mumewe Kabamba na ndugu wengine, wamekataa kuzungumzia chanzo cha tukio hilo, wakisisitiza kuwa wanaiachia mamlaka husika kufanya uchunguzi wake.

Kwa sasa, macho na masikio ya wengi yameelekezwa kwa Jeshi la Polisi kusubiri majibu ya uchunguzi yatakayotoa mwanga juu ya mauaji hayo.

Hata hivyo, itakuwa siku chache zilizopita, Mwananchi ilizungumza na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kuhusiana na mauaji hayo ambaye alisema mtuhumiwa amekamatwa na uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha tukio hilo.

Alisema madai yanayosambaa miongoni mwa wananchi kuhusu chanzo cha tukio hilo ni sehemu ya mambo yanayochunguzwa na polisi.

“Mtuhumiwa amekamatwa na uchunguzi unaendelea. Hicho kinachozungumzwa na wananchi ndicho pia tunakifanyia kazi,” alisema Muliro.

Kwa mujibu wa baadhi ya majirani na mashuhuda, tukio hilo linadaiwa kuhusishwa na mgogoro kati ya wadogo wawili wa marehemu, Lightness na Meshack, waliokuwa wakiishi katika nyumba moja na Linah, eneo la Rynes, Kigamboni.

Akielezea alivyolikuta tukio hilo, mjumbe wa shina namba sita wa Tawi la Mkwajuni, Kata ya Vijibweni, Aloyce Msiagi alisema alimkuta marehemu amelala chumbani sakafuni akiwa ametapakaa damu.

Alisema kisu kinachodaiwa kutumika kilikutwa chumbani juu ya kitanda, huku dalili zikionyesha marehemu alijeruhiwa awali kwenye korido kabla ya kuburuzwa hadi chumbani.

Kwa mujibu wa maelezo aliyoyapata kutoka kwa mdogo wa marehemu, tukio hilo lilianza pale mtuhumiwa alipodaiwa kumfuata dada yake mwingine jikoni akiwa na kisu akitaka kumshambulia. Binti huyo alikimbilia chumbani na kujifungia, ndipo Linah alipotoka kwenda kuangalia kilichokuwa kinaendelea.

“Inadaiwa walikutana koridoni ndipo akamchoma,” alisema Msiagi.

Aliongeza kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha sehemu mbalimbali ikiwamo shingoni na tumboni, huku mtuhumiwa naye akionekana kuwa na alama za kujitetea, hali inayoashiria kulikuwa na mapambano.

Mashuhuda wengine walidai kuwa mtuhumiwa alitoa maelezo yasiyoeleweka alipoulizwa na askari, akidai mara kuwa marehemu alimtumia watu wamtishe na wakati mwingine kutoa kauli zisizo na mwelekeo.

Jirani mmoja alidai chanzo cha ugomvi huo kinahusishwa na madai ya fedha kiasi cha Sh1.5 milioni ambazo mtuhumiwa alichukua kwa mteja bila kukamilisha mzigo.