Lukuvi alivyogusa maisha ya wananchi Idodi

Iringa. Kifo cha William Vangimembe Lukuvi (70) kimeibua simanzi kijijini kwao, Idodi, Jimbo la Islamani, mkoani Iringa kwa wananchi aliowaongoza kwa miaka zaidi ya 31 wakishikwa butwaa wasiamini kilichotokea.

Kifo hicho kimetangazwa leo Machi 25,2026 na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka juu ya msiba huo wa Lukuvi aliyezaliwa Agosti 15, 1955.

Mwananchi limefika katika Kijiji cha Idodi na kuzungumza na watu mbalimbali huku wananchi wakionekana kusimama makundi makundi kujadiliana juu ya msiba huo wa mbunge wao aliowaongoza tangu mwaka 1995.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Idodi, Christopher Chahe amesema hali ya wananchi kwa sasa si nzuri kutokana na msiba huo, kwani wengi wao wako katika majonzi makubwa na wanahisi wamepoteza mtu wa muhimu aliyekuwa akisimamia na kusukuma mbele maendeleo yao kwa vitendo.

“Wananchi wanapata shida kubwa sana kwa sasa, wako kwenye simanzi na bado hawaamini kilichotokea kutokana na mapenzi makubwa waliyokuwa nayo kwa kiongozi huyu,” amesema Chahe.

Chahe amesema kiongozi huyo alikuwa na nafasi ya kipekee katika jamii, kwani aliweza kujenga uhusiano wa karibu na wananchi na kushiriki nao katika shughuli mbalimbali za kijamii, jambo lililomfanya kupendwa na kuheshimiwa na watu wa rika zote.

Aidha, mwenyekiti huyo amesema katika kipindi chote cha uongozi wake, kiongozi huyo alisimamia na kusaidia utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa shule mpya na uboreshaji wa zilizokuwepo, hali iliyosaidia kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wa kijiji hicho.

“Alisaidia sana kujenga na kuboresha shule, watoto wetu walipata mazingira mazuri ya kusoma na kufikia ndoto zao,” amesema Chahe.

Katika sekta ya afya, amesema huduma ziliboreshwa kwa kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji uliofanyika katika vituo vya afya, hali iliyowarahisishia wananchi kupata matibabu bila kusafiri umbali mrefu kama ilivyokuwa hapo awali.

Hatuwezi kumsahau, aligusa maisha ya wengi wetu na ataendelea kuishi katika kumbukumbu zetu milele.”

“Sekta ya afya imeboreshwa, huduma zimekuwa karibu zaidi na wananchi na hii imeokoa maisha ya watu wengi,” amesema.

Akizungumza kwa majonzi, mkazi wa kijiji hicho, Christina Majani amesema msiba huo umeacha maumivu makubwa mioyoni mwa wananchi wengi, hasa ukizingatia waliwahi kunufaika na msaada wa mara kwa mara wa vyakula uliokuwa ukitolewa kwa lengo la kuwasaidia wananchi waliokuwa katika hali ngumu ya maisha, jambo ambalo lilionyesha kujali na kuwathamini.

Majani amesema mbali na misaada hiyo ya awali, juhudi za maendeleo ziliendelea kushika kasi baada ya kuanzishwa kwa skimu za umwagiliaji, ambazo ziliwasaidia wananchi wengi kuachana na kilimo cha kutegemea mvua na kuanza kulima kwa uhakika zaidi, hali iliyochangia kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato cha kaya nyingi kijijini hapo.

Kwa upande wake, Musa Kigelelo ambaye ni mwananchi wa Idodi na kiongozi mstaafu aliyewahi kuwa mwenyekiti wa kijiji hicho kwa miaka 27 iliyopita kuanzia mwaka 1993 hadi 2014, amesema kuwa msiba huo ni mzito sana kwa jamii nzima, kwani umeondoa mtu aliyekuwa nguzo muhimu katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya kijiji hicho kwa muda mrefu.

Kigelelo ameeleza katika kipindi chake cha uongozi, alishuhudia kwa karibu jitihada na mchango wa kiongozi huyo katika kuhamasisha na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, jambo ambalo lilileta mabadiliko chanya kwa wananchi wa Idodi na maeneo ya jirani.

“Huu ni msiba mzito sana kwa jamii yetu, tumepoteza mtu ambaye alikuwa msaada mkubwa katika maendeleo yetu na maisha ya wananchi wa kawaida,” amesema Kigelelo kwa masikitiko.

Naye Erick Kiponda, mkazi mwingine wa kijiji hicho, amesema bado wananchi wengi wanashindwa kuamini kilichotokea kutokana na namna walivyompenda na kumthamini kiongozi huyo, akieleza kuwa alikuwa karibu sana na wananchi na alisikiliza kero zao kwa ukaribu mkubwa.

“Inaumiza sana na bado ni vigumu kuamini kilichotokea, tulimpenda sana na alikuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku,” amesema Kiponda.

Brastus Fusi amegusia mchango wa kiongozi huyo katika kukuza sekta ya michezo kijijini hapo, akisema kuwa kupitia juhudi zake, vijana wengi walipata fursa ya kushiriki katika michezo mbalimbali, hali iliyosaidia kuwajenga kimwili na hata kuwafungulia fursa nyingine za maisha.

“Alifanya kazi kubwa sana katika sekta ya michezo, vijana walipata motisha na nafasi za kuonyesha vipaji vyao, jambo ambalo halikuwa rahisi kabla yake,” amesema Fusi.

Pamoja na mafanikio hayo yote, wananchi wanasema bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, na wana hofu bila uwepo wa kiongozi huyo, baadhi ya miradi inaweza kudumaa au kupoteza mwelekeo wake.

“Bila yeye mambo yatakuwa magumu zaidi, alikuwa anasimamia mengi kwa karibu sana,” amesema

mkazi mwingine kwa huzuni.

Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa kimetoa salamu za rambirambi juu ya kifo cha Lukuvi kikimtaja kuwa alikuwa nguzo muhimu ya chama na Taifa kwa ujumla.

Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM mkoani humo, Joseph Ryata amesema kifo cha Lukuvi ni pigo kubwa si tu kwa chama bali pia kwa wananchi wa Iringa na Tanzania kwa ujumla kutokana na mchango wake mkubwa wa maendeleo.

“Tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa hizi za msiba na Lukuvi alikuwa muhimili na alama ya CCM, si tu Iringa bali hata kitaifa kutokana na utendaji wake uliotukuka ndani ya chama na serikalini,” amesema Ryata.

Amesema chama hicho kinatoa pole kwa wanachama wake, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huo, huku kikiahidi kuendelea kutoa taarifa rasmi kuhusu taratibu za mazishi na kumuenzi kiongozi huyo.

“CCM itaendelea kuwapa taarifa wanachama wake kuhusu hatua mbalimbali za kuaga na kumuhifadhi mwanachama wetu,” ameongeza.