Mafunzo yaiwekea mkakati KVZ | Mwanaspoti

TIMU ya Mafunzo, imeanza kujinoa kwa ajili ya kumaliza vizuri msimu huu wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) katika mechi kumi zilizobaki ambapo itaanza na KVZ.

Akizungumza na Mwanaspoti kuelekea mchezo wao dhidi ya KVZ utakaopigwa Machi 28, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A, uliopo Mjini Unguja, Kocha Mkuu wa Mafunzo, Salum Ali Haji, ameweka wazi kuwa kikosi chake kiko tayari kupambana na kutoa upinzani mkali kutoka kwa wapinzani wanaowania ubingwa.

Alisema, anatambua kuwa KVZ wana kitu ambacho wanakitafuta kwakuwa wapo kwenye mbio za ubingwa, lakini hawawezi kukipata kwao.

“Mafunzo itakuwa timu ya kwanza kumsimamisha KVZ asielekee kuchukua ubingwa kwa sababu tunajipanga kushinda mechi hii tukiwa nyumbani,” alisema kocha huyo.

Hata hivyo, kocha huyo alisema kuelekea mchezo huo, kikosi hicho kitawakosa wachezaji wawili ambao ni Mikidadi aliyepata kadi za njano tatu pamoja na Jaku Joma aliyepata majeraha kwenye uwanja wa mazoezi.

Licha ya timu hiyo kukosa baadhi ya wachezaji kwenye mechi hiyo, kocha huyo alisema haijawa sababu ya kupoteza kwani wapo ambao wataziba nafasi hizo.

Pia, kocha huyo alisema timu inajizatiti kuhakikisha inashinda Kombe la FA na kucheza kwa ubora kwenye Kombe la Muungano mwaka huu.

“Tutaingia uwanjani kifua mbele na kujiamini, hatuna presha ya kushuka daraja lakini tunalenga kushinda na kumaliza katika nne bora ndani ya Ligi Kuu Zanzibar,” alisema Salum.

Kocha huyo, alisema timu hiyo imejiandaa kikamilifu kwa michuano inayoshiriki ikiwemo Ligi Kuu, FA Cup pamoja na Muungano Cup

Pamoja na changamoto hizo, kocha huyo alisema ana imani na kikosi chake kinaweza kufanya mazuri kwa sababu wapo wengi wanaoweza kazi.

Mafunzo ipo nafasi ya kumi katika msimamo wa ZPL ikivuna pointi 27 ikicheza mechi 20, imeruhusu mabao 16 na kufunga 20.

Msimu wa 2024-2025, timu hiyo ilimaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa ZPL ikiwa na pointi 30 ilizovuna kwenye mechi 30.