Mvutano kati ya Marekani na Iran umechukua sura mpya baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuanza kujiandaa kwa uvamizi wa ardhini kufuatia Tehran kukataa mpango wa amani uliowasilishwa hivi karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa za kijeshi, Marekani imetuma wanajeshi karibu 7,000 katika ukanda wa Mashariki ya Kati, wakiwemo askari wa anga kutoka kikosi cha 82nd Airborne pamoja na wanamaji, hatua inayotafsiriwa kama maandalizi ya operesheni kubwa ya kijeshi endapo mazungumzo yatashindikana.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesisitiza kuivamia upya Iran kufuatia Tehran kukataa mpango wa amani uliowasilishwa hivi karibuni. Picha na Mtandao
Mpango wa amani wa Trump uliokuwa na vipengele 15 ulihitaji Iran kufungua Mlango wa Hormuz, kusitisha mpango wake wa makombora ya masafa marefu pamoja na kuachana na shughuli za nyuklia. Hata hivyo, Iran imekataa masharti hayo na badala yake kutoa madai mazito, ikiwemo kufungwa kwa kambi zote za kijeshi za Marekani katika eneo la Ghuba, kuondolewa kwa vikwazo na kuendelea na programu yake ya makombora bila mipaka.
Mlango bahari wa Hormuz, ambao hupitisha takribani theluthi moja ya mafuta ya dunia ambao bado umeshikiriwa na Iran. Picha na Mtandao
Mlango wa Hormuz, ambao hupitisha takribani theluthi moja ya mafuta ya dunia, umeendelea kuwa kiini cha mgogoro huu, huku Iran ikitaka kuudhibiti na hata kutoza tozo kwa meli zinazopita hatua ambayo inaweza kubadilisha kabisa mizani ya nguvu kiuchumi na kisiasa katika ukanda huo.
Ndani ya utawala wa Trump, baadhi ya washauri wake wanasema rais huyo yuko tayari kwa mazungumzo lakini pia amejiandaa kwa hatua kali za kijeshi endapo Iran itaendelea kukaidi. Hata hivyo, maafisa wa Iran wameendelea kusisitiza kuwa hakuna mazungumzo ya moja kwa moja yaliyofanyika kati yao na Marekani.
Sehemu ya vikosi vya kijeshi vya Iran wakati vikiwa katika oparesheni ya kivita. Picha na Mtandao
Hali hii imeongeza wasiwasi kimataifa, hasa baada ya bei ya mafuta kupanda kwa kasi katika wiki za hivi karibuni kutokana na hofu ya kuvurugika kwa usambazaji kupitia Hormuz.
Kiongozi wa Bunge la Iran, Mohammad-Baqer Qalibaf, ambaye anaonekana kuwa na ushawishi mkubwa kwa sasa, amekanusha uwepo wa mazungumzo yoyote na Washington, akisisitiza msimamo wa nchi hiyo.
Sehemu ya mashambulizi ya mabomu katika mgogoro huo unaoendelea huko Mashariki ya Kati. Picha na Mtandao
Kadri hali inavyoendelea kuwa tete, dunia inaendelea kufuatilia kwa karibu kuona kama mgogoro huu utaishia mezani kwa mazungumzo au utageuka kuwa mzozo mkubwa zaidi wa kijeshi katika eneo hilo la Mashariki ya Kati.
Imeandikwa kwa msaada wa mtandao

