Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema yeyote atakayejitangaza kutoa huduma za tiba sili awe amesajiliwa.
Mchengerwa ametoa maagizo hayo kwenye banda la Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), alilotembelea katika mkutano wake na watoa huduma wa tiba asili unaofanyika Dodoma leo Jumatano, Machi 25, 2026.
Waziri huyo amesema lazima watu hao watambuliwe kwa kusajiliwa kwenye jumuiya za watafiti na watoa huduma za tiba asili.
Amesema wapo watu wanaoibuka wakisema ‘ukipata changamoto ya figo fanya hivi usiende hospitali’ haiwezekani. “Kama ni madaktari wawe wanatambulika na kama ni watoa huduma za asili lazima watambuliwe ili yule anayetoka akizungumzia tiba fulani tuwe tunamtambua.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwenye banda la Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), alilotembelea katika mkutano wake na watoa huduma wa tiba asili unaofanyika Dodoma leo Jumatano, Machi 25, 2026.
“Haiwezekani tukawa na Taifa ambalo kila mtu anasimama anasema yeye ni daktari, anatibu hiki na hiki. Tunapokea kesi nyingi za watu wa miaka 15, 16, 17 wanaugua figo kwa sababu hamjaweka utaratibu mzuri,” amesema.
Ameielekeza NIMR kumshughulikia yeyote atakayeibuka na kusema tiba fulani inasaidia kutibu ugonjwa fulani lakini hajasajiliwa.
“Maelekezo yangu ni kwamba wekeni utaratibu wa kuwatambua wataalamu wote wa tiba asili na sisi Serikali tutawalinda na yule atakayetoka kwenda kuzungumzia dawa lazima awe amepita kwenye mfumo wenu mnamtambua na dawa mmezipitia,” amesema.
Amesema NIMR inatakiwa kuhakikisha inawaambia Watanzania kuhusu dawa za asili inazozitengeneza ikiwemo ya mafua.
“Kunapoibuka changamoto na dawa mnazo msikae ndani tokeni waambieni Watanzania dawa zipo njooni mtumie, hata kama ni za kuponya au kuongeza kinga mwilini” amesema.
Katika kuhakikisha hilo Waziri Mchengerwa amesema wizara iwalipie watu wa tiba asili waende wakasome.
Utaratibu wa vyakula sahihi
Aidha, Mchengerwa amesema lazima Watanzania wakumbuke kula vyakula vya asili ili kuondokana na maradhi yanayosababishwa na ulaji wa vyakula vya kisasa akisema vinasababisha maradhi.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema Tanzania tiba asili inahudumia kwa asilimia 60, huku duniani ikihudumia kwa asilimia 80 ya wananchi wote akisema hata wanaokwenda hospitali wapo walioanzia huko.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akiwa kwenye banda la Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), alilotembelea katika mkutano wake na watoa huduma wa tiba asili unaofanyika Dodoma leo Jumatano, Machi 25, 2026.
Amesema kwa historia ya tiba asili inaendelea kukua siku hadi siku hadi pale Serikali ilipoweka mfumo wa kisheria kutambua ikiwemo kuwekwa kwenye sera ya afya pamoja na kuundwa kwa Baraza la tiba asili linalofuatilia dawa zinatumiwa.
“Mwaka jana tuligundua asilimia 17 ya dawa za asili zilichakachuliwa na waliofanya hivyo walikamatwa wakachukuliwa hatua stahiki, pia baraza liligundua asilimia 25 ya dawa za tiba asili zilikutwa na sumukuvu inayotokana na kutohifadhiwa vizuri,” amesema.
Akitolea mfano wa nchi za India na Korea kutumia tiba asili amesema inatokana na wataalamu wa tiba asili kusoma, hivyo na wizara inachukua hatua huku akisema zipo kozi za ngazi mbalimbali zinazotoa elimu ya tiba asili.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwenye banda la Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), alilotembelea katika mkutano wake na watoa huduma wa tiba asili unaofanyika Dodoma leo Jumatano, Machi 25, 2026.
Kuhusu alichokiagiza waziri kuhusu usajili wa watoa huduma ili watakaojitokeza wawe wamesajiliwa awali mtumishi wa NIMR, Emmanuel Peter alisema wamepokea maelekezo na kwenda kuyafanyia kazi.
