Mkandala ajifungia kuirejesha Coastal kibabe

KIUNGO mshambuliaji wa Coastal Union, Cleophas Mkandala amesema licha ya kiwango bora alichonacho kwa sasa, lakini hafurahishwi na matokeo ya jumla ya timu hiyo akikiri kuwa inahitajika nguvu ya ziada kujiweka pazuri.

Pia staa huyo ameelezea kwamba, matarajio yake ni kuona Coastal Union ikimaliza Ligi Kuu Bara msimu huu nafasi sita za juu kwenye msimamo.

Mkandala aliyewahi kukipiga timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara ikiwamo Tanzania Prisons, Azam FC, Dodoma Jiji na Kagera Sugar, kwa sasa anakinukisha kwa ‘Wagosi wa Kaya’.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkandala alisema licha ya kurejea na kiwango bora, lakini hafurahishwi na matokeo ya jumla ya timu hiyo akieleza kuwa wanaendelea kujitathmini namna ya kuondoka nafasi waliyopo.

Alisema kipindi hiki cha mapumziko wanaendelea kujisahihisha makosa na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi kuhakikisha wanaporejea uwanjani waanze kuuwasha moto upya.

“Nashukuru nimekuwa katika kiwango bora kwakuwa naongoza idadi ya mabao ndani ya timu na si kwamba mimi ni mshambuliaji asili, licha ya hivyo bado matokeo ya jumla ya timu si mazuri sana, lazima kipindi hiki tukitumie vyema.

“Nilikosa mechi takribani nne hadi tano baada ya kuumia, lakini nimerejea upya na nishukuru ushirikiano wa wenzangu kikosini, tunaendelea kujipanga ili mechi zinazofuata tuweze kufanya vizuri,” alisema nyota huyo.

Kuhusu matarajio yake msimu huu, Mkandala alisema anahitaji kuendeleza kasi ya ufungaji mabao na kuisaidia timu kumaliza nafasi sita za juu akieleza kuwa mechi zilizobaki wanaweza kufikia malengo.

Kiungo huyo msimu huu ndani ya Coastal Union amefunga jumla ya mabao matano yakiwamo mawili Ligi Kuu Bara na matatu Kombe la Shirikisho la CRDB akiwa ndiye nyota mwenye mabao mengi kikosini hapo.

Coastal Union iliyowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 1988 wakati inaitwa Ligi Daraja la Kwanza, msimu huu hali imeonekana kuwa ngumu kwani katika mechi 16 ilizocheza, imevuna pointi 15 na kuwa nafasi ya 13 kwenye msimamo.