Mwanza. Mtu mmoja amefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya kutokea ugomvi uliozuka kutokana na ushabiki wa mpira kati ya mashabiki wa timu za Simba na Yanga Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wilbrod Mutafungwa iliyotolewa leo Jumatano Machi 25, 2026 imeeleza kuwa Abel Mazuri (25) mkazi wa Nyamahengo aliuawa katika tukio hilo kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kifuani.
Mutafungwa amesema jeshi hilo limeanza msako wa kumtafuta kijana mmoja (jina limehifadhiwa kwa sasa) kwa tuhuma za mauaji hayo na kisha kuwajeruhi watu wawili kwa kutumia kitu chenye ncha kali, walipokuwa wanakunywa pombe na kuangalia mpira kwenye banda la maonyesho ya mpira, katika kata ya Sumve, wilayani Kwimba.
Amesema tukio hilo limetokea Machi 24, 2026, saa 5:30 usiku, katika kitongoji cha Nyamahengo ambapo inadaiwa kuwa mtuhumiwa aliwashambulia na kuwajeruhi watu watatu kwa kutumia kitu chenye ncha kali kufuatia ugomvi uliotokana na ushabiki wa mpira kati ya timu ya Simba na Yanga na kusababisha mauaji hayo.
Waliojeruhiwa katika tukio hilo ni Semen Cherehani (26) na Ndubu Chagula (26) wote wakazi wa kijiji cha Sumve na walishambuliwa maeneo ya mkononi.
“Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha shambulio hilo ni ushabiki wa mpira uliovuka mipaka na kuleta ubishani mkali kati ya mashabiki wa klabu za Simba na Yanga.”
“Waathirika wote wamepatiwa fomu za matibabu ya Polisi (PF3) na hivi sasa wanapata matibabu katika Hospitali Teule ya Sumve,”amesema Mutafungwa.
Ameeleza hali zao zinaendelea kuimarika na Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada za kumtia mbaroni mtuhumiwa ili afikishwe katika vyombo vya sheria.
Katika tukio lingine, jeshi hilo linafanya uchunguzi sambamba na kumsaka mwanamke mmoja ambaye bado hajafahamika anuani ya makazi yake kwa tuhuma ya kumtupa mtoto mchanga baada ya kujifungua, anayekadiriwa kuwa na umri wa siku moja tangu kuzaliwa.
Tukio hilo limetokea Machi 24, 2026 saa 11:00 jioni katika Kitongoji cha Igudija, Kijiji cha Kitumba, Kata ya Kisesa, Wilaya ya Magu.
“Jeshi la Polisi lilipata taarifa za kutelekezwa kwa mtoto mchanga wa jinsia ya kiume kwenye jengo la nyumba ambalo ujenzi wake haujakamilika,
“Juhudi za kuokoa uhai wa mtoto huyo zilifanyika kwa bahati mbaya alifariki dunia,”amesema Mutafungwa.