Mnyika Afichua Mapya Zuio la Chadema Mahakama ya Rufaa Dodoma

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, amesema mwenendo wa shauri la marejeo ya kesi ya mgawanyo wa mali za chama umeanza kufichua ukweli kuhusu tafsiri halisi ya amri ya zuio iliyotolewa Juni 10, 2025.

Akizungumza baada ya kusikilizwa kwa shauri hilo Machi 24, 2026 katika Mahakama ya Rufaa Tanzania jijini Dodoma, Mnyika alisema hoja iliyotolewa na Wakili Saidi Marijani kwa niaba ya upande wa kina Saidi Issa Mohamed imethibitisha kuwa zuio hilo lilikuwa na mipaka maalum.

Kwa mujibu wa Mnyika, wakili huyo alieleza mahakamani kuwa zuio la kufanya shughuli za kisiasa lilimhusu Katibu Mkuu wa CHADEMA pamoja na Bodi ya Wadhamini pekee.

Aidha, zuio la matumizi ya mali za chama lilielekezwa kwa Katibu Mkuu, Bodi ya Wadhamini, wafanyakazi walio chini yake, mawakala wake na watu wanaotekeleza majukumu kwa maelekezo yake.

Mnyika amesema kuwa wakili huyo alisisitiza kuwa mtu yeyote ambaye hayuko chini ya Katibu Mkuu hakuwa amezuiwa kisheria kutumia mali za chama au kushiriki shughuli za kisiasa.

Hata hivyo, amesema kauli hiyo inakinzana na msimamo uliowahi kutolewa kwa umma na upande huo mwaka 2025, ambapo walidai zuio hilo liliwahusu viongozi wote wa chama pamoja na wanachama kwa ujumla.

Ameongeza kuwa hata waliwahi kumwandikia msajili wa Mahakama Kuu Tanzania wakidai kuwa CHADEMA wameupotosha umma kuhusu tafsiri ya zuio hilo, hatua iliyosababisha msajili kutoa ufafanuzi kuwa zuio hilo lingeweza kuwahusu viongozi wote.

“Leo wameyaruka maneno yao mbele ya Mahakama ya Rufaa,” amesema Mnyika, akisisitiza kuwa hali hiyo inaonesha wazi kuwa msimamo wa CHADEMA walioutoa mwaka 2025 ulikuwa sahihi.

Amesema maendeleo ya leo mahakamani yanawapa nguvu wanachama na viongozi wa chama hicho kuendelea na shughuli za kisiasa, akisisitiza kuwa hakuna zuio la kisheria linalowazuia wanachama au viongozi kushiriki shughuli hizo nje ya wale waliotajwa moja kwa moja kwenye amri hiyo.