YANGA imetangaza imemrudisha Abdihamid Moalin na kumwongeza katika benchi la ufundi la timu hiyo kuwa msaidizi wa Pedro Goncalves ambaye inaelezwa anahesabu siku katika klabu hiyo kutokana na kile kilichobainishwa aina ya uchezaji wa Yanga hauendani na wachezaji waliopo.
Uamuzi huo umekuja baada ya kikazo kizito kilichofanywa na uongozi wa Yanga juzi Jumatatu ukiongozwa na rais wake, Hersi Said na Pedro aliwasilisha ripoti ya tathmini ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
Taarifa ya Yanga imeeleza, kikosi chao kinakabiliwa na changamoto ya kukosa uwiano sahihi wa uchezaji, hali iliyochangia matokeo yasiyoridhisha na ndiyo maana wameamua kumrejesha Moalin.
Uamuzi huo walioufikia juzi Jumatatu baada ya kukutana na kocha wa kikosi hicho, Pedro Goncalves, umeonyesha wazi kulenga kuongeza nguvu ya kiufundi kwenye kikosi hicho ambacho kimetoa sare tatu mfululizo kabla ya mapumziko ya kalenda ya FIFA.
Yanga imeamua kumteua Moallin kuwa kocha msaidizi chini ya Pedro, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza nguvu ya kiufundi kwenye benchi la ufundi.
Kwa maneno mengine, Pedro ni kama yupo mtegoni kutokana na mwenendo wa klabu hiyo. Hata hivyo, Moallin ni mzoefu na ndiye aliyeongoza timu hiyo kwa kipindi fulani baada ya kuondoka ghafla kwa Sead Ramovic.
Moalin amewahi kuhudumu Yanga kama Mkurugenzi wa Ufundi na Kocha Msaidizi katika vipindi tofauti msimu uliopita 2024-2025 chini ya Kocha Sead Ramovic na Miloud Hamdi na kupata mafanikio ya kushinda Kombe la Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB na Kombe la Muungano 2025.
Katika kikao hicho, Pedro aliwasilisha hoja kadhaa muhimu zinazofafanua changamoto za timu hiyo, ikiwemo ratiba ngumu, majeraha ya baadhi ya wachezaji muhimu pamoja na masuala ya mbinu.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Yanga iliridhishwa na sababu hizo pia imeangalia kama ikivunja mkataba wa kocha huyo akiwa amebakisha miezi mitatu kabla ya mkataba wake kumalizika.
Chanzo hicho kilisema, Yanga imekwepa gharama kubwa za kuvunja mkataba wa makocha waliopo, hivyo wameamua kuendelea nao, huku wakimleta kocha ambaye atafanya mabadiliko ya haraka katika kipindi hiki kigumu.
“Tukiwa na uhalisia ni ngumu kumhukumu moja kwa moja Pedro, uzuri ni wote tumeona hali ya timu, hivyo viongozi walikubaliana naye na kwa kuwa bado timu ipo kileleni kuna mambo ya kuyafanyia kazi ili kufanya vizuri zaidi katika mechi zilizosalia na kutetea tena ubingwa wa Ligi.
“Lakini uongozi umeona ndani ya msimu mmoja kuachana na makocha wawili kuna gharama za kuvunja mikataba, tuliachana na Romain Folz, hatuwezi kuachana na Pedro wakati tunaona msimu unakwenda mwisho. Tukimaliza msimu tunaweza kufanya uamuzi.”
Chanzo hicho ambacho hakikutaka kuwekwa wazi, kiliongeza kwa kusema: “Kikao cha Jumatatu kilikuwa kikao cha kujenga zaidi na kilikuwa na mwelezo mzuri, hivyo kila kitu kipo sawa labda kuwe na mabadiliko mengine kwa sababu vikao hivi ni endelevu vyenye lengo la kuongeza ufanisi wa timu japo kulikuwa na presha kwa baadhi ya viongozi kutokana na kiwango cha timu.”
Katika taarifa yake, Yanga iliongelea suala la ratiba na majeruhi kwa kusema: “Ndani ya siku 21, kikosi chetu kimecheza michezo 7 mfululizo, michezo sita ya Ligi Kuu na mchezo mmoja wa Kombe la Shirikisho la CRDB.
“Ratiba hii pia ilijumlisha safari ya umbali wa Kilomita 4,462 kutoka Mkoa mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya mechi za ugenini. Uongozi unaamini safari hizi na ratiba kubana kulipunguza ufanisi wa wachezaji kutokana na uchovu uliopatikana.”
Kuhusu Majeraha, Yanga ilisema: “Mpaka sasa, timu yetu ina wachezaji nane muhimu ambao wamepata majeraha tofauti tofauti yaliowapelekea kukosa michezo. Khomein Aboubakar, Clement Mzize, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Chadrack Boka, Edmund John, Prince Dube na Laurindo Maria ‘Depu’. Wachezaji watatu kwenye orodha hii wamepata majeraha yatakayowaweka nje mpaka mwisho wa msimu.”
Aidha, licha ya changamoto hizo, uongozi pia ulisema umegundua uwepo wa changamoto ya kiufundi inayoifanya timu icheze aina tofauti ya uchezaji (style of play) na ile ambayo imezoelekea na kuendana na wachezaji walio ndani ya kikosi. Changamoto hiyo ya kiufundi imekuwa sababu ya kuifanya timu kupata wakati mgumu kupata matokeo mazuri na kucheza vizuri pia kwenye baadhi ya michezo ya Ligi Kuu.
