Kauli ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Abubakary Zubery imeibua tafakuri pana kuhusu umuhimu wa kulinda mshikamano wa kidini nchini, hasa katika nyakati hizi ambazo taarifa potofu na uchochezi vinaweza kusambaa kwa kasi kubwa.
Akizungumza katika Baraza la Idd El-Fitr lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mufti alitoa msimamo ulio wazi kwamba wapo watu wanaochochea migawanyiko ya kidini kwa makusudi, lakini si wawakilishi halisi wa dini zao.
Katika hotuba yake, Mufti alisisitiza mafundisho ya Uislamu yanahimiza uadilifu, uvumilivu na kuishi kwa amani na watu wa imani nyingine. Alieleza kuwa vitendo vya kubeza au kudhalilisha dini nyingine havipaswi kuhusishwa na waumini wa kweli, bali ni matokeo ya watu wachache wenye nia ya kuchochea migogoro. Kwa mantiki hiyo, aliwataka Waislamu kutokubali kuchokozwa na kauli au vitendo vinavyolenga kuvuruga mshikamano wa jamii.
Kauli hii inakuja katika wakati ambao mitandao ya kijamii imekuwa uwanja mpana wa mijadala mikali, mara nyingi ikichochewa na taarifa zisizo na uthibitisho.
Mufti alionya kuhusu matumizi ya teknolojia, ikiwamo akili mnemba (AI), katika kuzalisha taarifa za uongo zinazoweza kuibua taharuki na chuki. Hili ni onyo muhimu katika enzi ya kidijitali, ambapo ukweli unaweza kupotoshwa kwa urahisi na kusambazwa kwa kasi kubwa.
Aidha, Mufti aliwahimiza viongozi wa dini kuendelea kuwaombea viongozi wa nchi, akisisitiza nafasi yao katika kuimarisha maadili na mshikamano wa taifa.
Alikumbusha kuwa dini badala ya kuwa chanzo cha mgawanyiko, inapaswa kuwa daraja la kuunganisha watu.
Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan, alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na heshima miongoni mwa Watanzania.
Alieleza kuwa misingi hiyo ndiyo nguzo ya maendeleo ya taifa na kwamba, amani iliyopo ni matokeo ya juhudi za pamoja za wananchi na uongozi unaozingatia misingi ya kuheshimiana.
Rais Samia alibainisha wazi kuwa Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa Katiba, huku akionya dhidi ya matumizi mabaya ya uhuru huo.
Alisisitiza kuwa uhuru wa dini unapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji, ili kuepusha vitendo vinavyoweza kuchochea migawanyiko au kuvuruga amani ya nchi.
Kauli yake kwamba “tofauti zetu kiimani zijenge daraja la kuimarisha udugu wa Watanzania”, inaakisi dhamira ya kuendeleza utamaduni wa kuvumiliana na kuheshimiana. Ni wito unaohitaji kutafsiriwa kwa vitendo, hasa katika kipindi ambacho baadhi ya mijadala ya kijamii imeonekana kuchukua sura ya kidini.
Rais pia alitambua mchango wa viongozi wa dini katika kujenga maadili ya jamii, akieleza kuwa wamekuwa nguzo muhimu ya kudumisha utulivu wa nchi. Hata hivyo, alikemea vitendo au kauli zinazoweza kuchochea chuki na uhasama, akionya kuwa hazina nafasi katika taifa lenye historia ya umoja na amani.
Hata hivyo, hali ilivyo sasa inaonyesha kuwepo kwa changamoto mpya. Katika kipindi cha hivi karibuni, baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakitoa kauli au nyaraka zenye mwelekeo mkali kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kauli hizo zimechochea mijadala mikali miongoni mwa wafuasi wao, hasa kwenye mitandao ya kijamii na wakati mwingine kuonekana kana kwamba ni mvutano wa kidini.
Lakini ukweli unabaki kuwa Tanzania haina mgogoro wa kidini. Ni taifa lisilo na dini rasmi huku Katiba ya mwaka 1977, kupitia Ibara ya 19, ikitoa uhuru kwa kila mtu kuamini, kuabudu na kueneza dini yake bila kuingiliwa.
Mfumo huu umewezesha Watanzania kuishi kwa muda mrefu katika hali ya kuvumiliana licha ya tofauti zao za kiimani.
Ndiyo maana kauli za Mufti na Rais Samia zinapaswa kuangaliwa kama mwongozo muhimu katika kipindi hiki. Zinakumbusha kuwa tofauti za dini si chanzo cha mgawanyiko, bali ni fursa ya kujenga mshikamano zaidi.
Kwa ujumla, wajibu wa kulinda amani na mshikamano haupaswi kuachwa mikononi mwa viongozi pekee. Kila Mtanzania ana nafasi yake katika kuhakikisha kuwa lugha, vitendo na mitazamo yake haviwi chanzo cha migawanyiko. Ni muhimu kuwa makini na taarifa tunazopokea na kusambaza, pamoja na kuepuka kuingia kwenye mijadala yenye lengo la kuchochea chuki.
Katika taifa lenye historia ya kuishi kwa amani kama Tanzania, ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa urithi huo unaendelea kudumishwa. Wachochezi wa migawanyiko hawapaswi kupewa nafasi, iwe wanatoka upande wowote.
Ujumbe uliotolewa na viongozi hawa unaweka bayana kuwa mshikamano wa kitaifa ni nguzo isiyopaswa kuyumba. Kulinda amani ni jukumu la wote na kuanza na kila mmoja wetu.
