Mbeya. Mvua kubwa inayoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini imesababisha maafa ya vifo vya watu 18 kati yao 14 ni watoto Kata ya Nkunga, Lupepo, Kawetele na Ikuti wilayani Rungwe.
Vifo hivyo vimetokea kati ya saa 6 hadi 9:30 usiku wa kuamkia leo Jumatano, Machi 25, 2026 baada ya mvua iliyokuwa na upepo kusababisha nyumba zaidi ya tisa zilizojengwa kwa tofali ambazo hazijachomwa na kuezekwa bati kusombwa na maporomoko ya udongo na kusababisha vifo hivyo.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya imesema kati ya waliofariki dunia 14 ni watoto ambao wanane ni wa kike na sita wa kiume. Watu wazima ni wanne ambapo watatu ni wanawake na mmoja ni mwanaume.
Waliofariki dunia wametajwa ni Chapakazi Mwasota (60), Rhoida Mwangwina (55), Gladness Chapakazi (18), Neema Mwasyema (31), Aneth Morohan (35), Obeid Shibuka (20) na Itika Manyanya (26).
Watoto waliofariki ni Vivian Ahonga (1), Briana Mwachiombo (3), Dailan Kasambala (6) aliyekuwa mwanafunzi wa chekechea katika Shule ya Msingi Lupepo, Innoent Kasambala (4), Vivian Andrea (13) aliyekuwa mwanafunzi darasa la saba Shule ya Msingi Lupepo na Princess Ibrahim (5) aliyekuwa mwanafunzi wa chekechea Shule ya Msingi Lupepo.
Wengine ni Nathanael Christopher (2), Jonathan Hamis (miezi 10), lrine Anangisye (16) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Lupepo, Wema Hamis (5), aliyekuwa Mwanafunzi wa Chekechea Shule ya Msingi Kikuyu na Kenedy Mahenge (14), aliyekuwa Mwanafunzi wa Kidato cha Pili Sekondari ya Ikuti.
Aidha, Polisi wamesela katika maafa hayo watu watano walijeruhiwa kati yao watoto watatu wa kike na watu wazima wawili, mwanaume mmoja na mwanamke mmoja.
Polisi wamesema majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya Makandana — Tukuyu na Zahanati ya Chuo cha Magereza Kiwira.
Polisi wamesema kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wanaendelea na kazi ya uokoaji katika maeneo hayo.
“Timu za madaktari zipo amebei hayo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kitabibu wa miili ya marehemu na kutoa huduma za awali kwa waathirika,” imeeleza taarifa hiyo.
